Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Hussein Ngaga. |
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
OFISA ushirika wa wilaya ya Mbinga
mkoani Ruvuma, Raphael Luvanda amejikuta akiwa katika wakati mgumu kufuatia Wanachama
wa chama cha kuweka na kukopa, Mbinga Lutheran SACCOS kilichopo wilayani humo kumjia
juu na kumweleza kwamba hawana imani naye katika utendaji wa kazi zake, hivyo
hawamtaki kumuona akifanya kazi za ukaguzi katika umoja huo.
Sambamba na hilo wanachama hao ambao
walionekana kukerwa na tabia za Ofisa ushirika huyo walisema, sababu zao za
msingi za kumkataa wamekuwa wakimtuhumu kwa muda mrefu kwamba anafanya kazi
zake kwa mrengo wa kushoto kwa kutofuata taratibu husika.
Walieleza kuwa bodi husika
itazifikisha tuhuma husika kwa mwajiri wake ambaye ni Mkurugenzi mtendaji wa
Halmashauri ya wilaya Mbinga, ili ziweze kufanyiwa kazi huku wakitaka kuanzia
sasa shughuli za ukaguzi zifanywe na ofisa ushirika mwingine kutoka katika
halmashauri hiyo na sio vinginevyo.
Hali hiyo ya wanachama hao kumtuhumu
Ofisa ushirika huyo ilijitokeza katika mkutano mkuu wa wanachama, liofanyika kwenye
ukumbi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) uliopo mjini hapa.
Walisema katika hali ya kusikitisha
Luvanda amekuwa na tabia za kupenda kuzua migogoro ya hapa na pale kati ya
uongozi wa SACCOS hiyo na wanachama kwa ujumla.
Vilevile katika taarifa yake ya
ukaguzi ya mwaka 2013 alishindwa kubainisha wizi wa fedha uliofanywa na
aliyekuwa mhasibu wa ushirika huo, Ansilla Kapinga na kusababisha uongozi
husika kutumia gharama kubwa kuleta wakaguzi wengine kutoka nje ya wilaya ya
Mbinga.
Waliongeza kuwa amefikia hatua, hata
vitabu na nyaraka muhimu za umoja huo amezuia ofisini kwake akitaa kuzirejesha,
jambo ambalo limekuwa likizua malalamiko ya hapa na pale miongoni mwa wanachama
na kufanya wakose imani naye.
“Kwa mwenendo huu hatutaweza kuvumilia
suala hili, ni vyema Ofisa ushirika huyu afanye kazi zake kwa kufuata taratibu
zilizowekwa na sio kujenga mipasuko ambayo inavuruga ushirika wetu”, walisema.
Walifafanua kuwa wanazo taarifa
kwamba, Luvanda amekuwa hata akitoa taarifa za upotoshaji kwenye maeneo mengine
ya mashirika ambayo yanatoa mikopo hapa wilayani, kwa lengo la kugonganisha
viongozi husika na wanachama kwa maslahi yake binafsi.
Hata hivyo kwa upande wake Ofisa
ushirika huyo alipopewa nafasi ya kujieleza aliishia kwa kuwaomba radhi
wanachama hao, na kuondoka bila kutolea maelezo yakinifu yenye kufikia muafaka
wa tuhuma ambazo alikuwa akinyoshewa kidole katika mkutano huo.
No comments:
Post a Comment