Na
Kassian Nyandindi,
Mbinga.
MKURUGENZI
mkuu wa bodi ya kahawa Tanzania (TCB) Adolf
Kumburu ameziasa Halmashauri na taasisi mbalimbali hapa nchini ambako
zao la kahawa linazalishwa, kuhakikisha kwamba wanashiriki kikamilifu katika
kuzalisha miche bora ya kahawa ili kuweza kuwafikia wakulima walio wengi
kiurahisi na kukua kwa uzalishaji wa zao hilo.
Alisema
pamoja na Taasisi ya utafiti wa kahawa nchini (TaCRI) kuzalisha miche hiyo na kuisambaza,
bado haitoshelezi mahitaji, kutokana na uzalishaji kuwa mdogo hivyo ili
kuondokana na tatizo hilo
wakulima, halmashauri na taasisi zingine zinapaswa kushiriki katika kuanzisha
bustani mama za kuzalishia miche ya kahawa.
Alifafanua
kuwa wakulima walio wengi tayari walishajengewa
uwezo na wataalamu wa TaCRI namna ya kuzalisha miche, hivyo hawana budi kutumia
utaalamu husika waliopewa katika kuifanya kazi hiyo ili kuondokana na tatizo la
upatikanaji wa miche hiyo.
Kumburu
aliyasema hayo wakati wa kikao cha wadau wa kahawa Kanda ya Ruvuma,
kilichoketi kwenye ukumbi wa Jimbo Katoliki mjini hapa.
Aidha
alieleza kuwa malengo ya nchi katika kuongeza uzalishaji wa kahawa ni kufikia
tani 80,000 mwaka 2016 na tani 100,000 mwaka 2021 ambapo katika kufanikisha
hilo ni lazima elimu ya kutosha iwafikie wakulima sambamba na matumizi ya
pembejeo (mbolea) za kutosha katika mashamba yao.
“Makisio
ya uzalishaji wa kahawa mwaka huu ni tani 61,800 mara nyingi malengo ya
uzalishaji hatufikii kutokana na changamoto kubwa ya matumizi madogo ya
pembejeo za kilimo hasa mbolea”, alisema Kumburu.
Kwa
upande wa masoko Mkurugenzi huyo alisema asilimia 85 hadi 90 ya wakulima wadogo
wadogo, wanatumia soko la mnada na kwamba asilimia kumi inayobakia wakulima hao
hupeleka kahawa yao
moja kwa moja katika soko la nje.
Pamoja
na mambo mengine aliongeza kwamba ili kahawa iweze kupata bei nzuri katika soko
la ndani au nje, akulima wanapaswa kuzingatia suala la ubora ikiwemo kuzingatia
kanuni za kilimo bora cha zao la kahawa.
Kumburu
alisema katika Afrika, Tanzania ni nchi ya nne kwa uzalishaji wa kahawa ambapo
huzalisha magunia milioni moja kwa msimu mmoja wa kilimo cha zao hilo, ambapo
nchi inayoongoza ni Ethiopia ambayo inazalisha magunia milioni 5 ikifuatiwa na
Uganda inayozalisha magunia milioni 3 na nchi ya tatu ni Ivory Coast huzalisha
magunia milioni 1.5.
No comments:
Post a Comment