Na Kassian Nyandindi,
Songea.
ASKARI watatu wa Jeshi la Polisi mkoani Ruvuma,
wamelazwa katika hospitali ya mkoa huo iliyopo Songea mjini wakiwa
wanapatiwa matibabu baada ya kushambuliwa na kitu kinachodaiwa kuwa ni bomu la
kurusha kwa mkono.
Tukio hilo limetokea Septemba 16 mwaka huu majira ya
jioni katika kata ya Msufini mjini hapa, ambapo wamejeruhiwa.
Akizungumzia tukio hilo kaimu kamanda wa polisi wa
mkoa huo ASP George Chiposi, alisema kuwa watu watatu wasio fahamika ndio
waliotupa kitu hicho kinacho sadikiwa kuwa ni bomu la kutupwa kwa mkono.
Bomu hilo alisema limetengenezwa kienyeji na
kuwajeruhi askari hao watatu waliokuwa doria.
Kamanda Chiposi aliwataja askari hao waliojeruhiwa
kuwa ni WP. 10399 PC Felista ambaye amejeruhiwa mguu wa kulia
kwenye unyayo na pajani, G. 7351 PC Ramadhani aliye jeruhiwa mguu wa
kulia karibu na goti na tumboni upande wa kulia na G. 5515 pc John
aliyepata majeraha katika mguu wa kulia chini ya goti na jeraha dogo tumboni.
Alisema baada ya tukio hilo majeruhi wote walikimbizwa
katika hospitali hiyo ya mkoa, na wote wamelazwa huko wakiendelea
kupatiwa matibabu.
Alifafanua kuwa katika matibabu ya awali waganga (madaktari)
wameweza kutoa vipande vya bati na misumari katika majeraha ya askari hao na
mpaka sasa wanaendelea vizuri.
Chanzo cha tukio hilo mpaka sasa bado hakijafahamika
na akaongeza kuwa uchunguzi wa awali uliofanywa katika eneo la tukio
walifanikiwa kuokota vipande vya chuma, kopo lenye nyaya, kipande cha ganda la
betri ambavyo vinasadikiwa ndivyo vilikuwa sehemu ya bomu hilo.
Kufutia hali hiyo Jeshi la polisi mkoani Ruvuma,
linaendelea na uchunguzi wa ili kuweza kuwakamata wahusika wa tukio hilo
kwa hatua zaidi za kisheria.
No comments:
Post a Comment