Na Mwandishi wetu,
Songea.
MKUU wa mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu
amekipongeza chuo kikuu cha sayansi ya kompyuta cha Mtakatifu Joseph tawi la
Songea mkoani humo, kwa jitihada zake za kuendelea kupanua wigo wa kutoa huduma
na kukuza elimu ya juu hapa nchini.
Mwambungu alitoa pongezi hizo alipokuwa
akihutubia kwenye mahafali ya tano ya chuo hicho mjini hapa, kwa wahitimu 119
wa shahada na stashahada ambapo alisema kuwa kuanzishwa kwa chuo hicho,
kumesaidia kulipunguzia taifa tatizo la ukosefu wa wataalam wa sayansi hususan
katika ukanda wa kusini na taifa kwa ujumla.
Alisema kuwa kuanzishwa kwa chuo kikuu cha
sayansi ya kilimo na teknolojia katika sekta ya kilimo, ni jambo jema kwa
ustawi wa nchi na uti wa mgongo na mwajiri mkubwa kwa wananchi huku akiwataka
wahitimu hao kutumia elimu waliyoipata kwa ajili ya kuleta mabadiliko chanya katika
jamii.
Alieleza kuwa katika maisha ya sasa hakuna njia
fupi ya kufikia mafanikio katika maisha zaidi ya kufanya kazi kwa bidii
na maarifa, na kwamba changamoto zilizopo katika chuo hicho zigeuzwe kuwa fursa
pekee ya kujipanua na kutoa elimu bora, huku akiwataka kuboresha
mawasiliano ili kukuza wigo wa utatuzi wa changamoto hizo.
Vilevile Mkuu huyo wa mkoa wa Ruvuma, aliwataka wanafunzi
wa chuo hicho cha Mtakatifu Joseph, kuombea amani hususan katika kipindi hiki
kigumu ambacho Taifa linaingia kwenye mchakato wa uundwaji wa katiba mpya, na
kwamba wajiepushe na wale wenye tabia ya kuhamasisha uvunjifu wa amani bila sababu
za msingi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa bodi ya ushauri ya
chuo hicho Askofu John Ndimbo, alisema anajisikia fahari kuona chuo hicho
kinazalisha wataalam wengi wa sayansi kanda wa kusini, huku akisema kuwa elimu
ni tunu kubwa ya maendeleo katika ulimwengu wa sasa wa karne hii ya sayansi na
tekinolojia.
Ndimbo alitoa rai kwa uongozi wa chuo na wanafunzi
kuhakikisha wanafuata taratibu, sheria na miongozo ya wizara ya elimu badala ya
kuzalisha migogoro isiyokuwa na faida yoyote kwa madai kwamba, gharama ya
kutuliza ni kubwa pamoja na kupoteza rasilimali muda.
No comments:
Post a Comment