Na Kassian Nyandindi,
Ruvuma.
SERIKALI hapa nchini imeruhusu wafanyabiashara kuuza mahindi
yao nje ya nchi popote pale, huku ikiwataka kuzingatia bei elekezi iliyowekwa ili
kumfanya mkulima asiweze kupata hasara.
Sambamba na hilo mahindi ambayo yamehifadhiwa katika vituo
husika vilivyopo mkoani humo, serikali itayanunua kwa kilo shilingi 500 na
kwamba wakulima hawaruhusiwi kuingiza mahindi mengine katika vituo.
Mkurugenzi wa mipango na uendeshaji kutoka makao makuu ya
mamlaka ya hifadhi ya chakula Tanzania (NFRA), Anna Ngoo alisema hayo wakati
alipokuwa katika ziara yake ya kikazi mkoani Ruvuma akikagua mahindi ambayo
yamehifadhiwa katika vituo husika mkoani humo.
“Mahindi yaliyopo sasa katika vituo hivi vya kununulia yasiingizwe
tena, serikali ipo tayari kuyanunua haya tu yaliyopo sasa”, alisisitiza.
Vilevile Ngoo aliwataka
wakulima hapa nchini katika maeneo ambayo mahindi yanazalishwa kwa wingi, wajiunge
katika vikundi ili serikali iweze kununua zao hilo kwa urahisi.
“Wakulima hawa wakiwa pamoja na serikali ikatekeleza majukumu
yake hizi kelele za kutaka tununue mahindi yote waliyozalisha hazitakuwepo tena,
tuwaelimishe wajiunge pamoja”, alisema Ngoo.
No comments:
Post a Comment