Rais Jakaya Kikwete wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania. |
Na Kassian Nyandindi,
Ruvuma.
JESHI la Polisi
nchini limetakiwa kuacha vitendo vya
kuwanyanyasa waandishi wa habari na kuwafanya wasitekeleze wajibu wao
ipasavyo, kufanya hivyo ni kutowatendea haki na kudhalilisha taaluma ya habari.
Sambamba na hilo Jeshi
hilo limenyoshewa kidole kwamba limekuwa na historia ya kupiga na kuwafukuza
waandishi wa habari, hasa pale wanapotafuta ukweli juu ya matukio mbalimbali
ambayo yamekuwa yakitokea miongoni mwa jamii.
Rai hiyo imetolewa
na baadhi ya Wananchi wa mkoa wa Ruvuma, walipokuwa wakizungumza na mwandishi
wa habari hizi kwa nyakati tofauti kufuatia tukio lililotokea jana makao makuu
ya jeshi hilo baada ya waandishi kupigwa, kukimbizwa na mbwa ili wasichukue
taarifa za kuhojiwa kwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(CHADEMA) Freeman Mbowe.
Walisema tukio la
kupigwa na kudhalilishwa kwa waandishi wa habari ni ishara tosha ya polisi
waliofanya kitendo hicho kutoheshimu taaluma ya habari, huku wakivitaka vyombo
mbalimbali vya kutetea haki za binadamu kuchukua hatua za kisheria dhidi ya
askari polisi waliofanya kitendo hicho.
Richard Haulle
mkazi wa Mpandangindo wilaya ya Songea vijijini mkoani humo, alisema Waandishi
wa habari ni mhimili pekee ambao unategemewa hapa duniani kwa kutoa taarifa
mbalimbali, juu ya nini kinachoendelea katika ulimwengu wa sasa hivyo jamii
inapaswa kuendelea kuwaheshimu hasa pale wanapokuwa wakitimiza majukumu yao ya
kazi za kila siku.
Alieleza kuwa
Tanzania ni nchi yenye amani, hivyo kufikia hatua ya muendelezo wa kupiga waandishi
ni kujenga tabaka la kuharibu amani tuliyonayo kama alivyosema hivi karibuni Makamu
wa Rais Dokta Mohamed Gharib Bilal, kuvitaka vyombo vya ulinzi na usalama
nchini kushirikiana na waandishi wa habari katika kufanya kazi kwa ajili ya
kulinda amani ya nchi.
David Ndunguru
mkazi wa kata ya Litembo wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma alisema, “ni kitendo cha ajabu sana kuona polisi
wanawapiga mabomu ya machozi waandishi, wanawafukuzwa na mbwa utafikiri kama ni
wahalifu ni vizuri sasa hata kama kuna amri inatoka kwa kiongozi wa juu wajirekebishe
huu sio utawala bora”.
Ndunguru alisema
kuwa Paul Chagonja ambaye ni Kamishna wa Operesheni na Mafunzo anapaswa
kushushiwa lawama nzito, kutokana na muda mwingi alikuwa akionekana akiwaagiza
askari wake wawaondoe waandishi wasitekeleze majukumu yao na hata kuwasakizia
mbwa.
Kadhalika Hashimu
Rashid mkazi wa Songea mjini naye alilaani juu ya vitendo hivyo, ambapo
alifafanua kuwa hali hiyo ni kuminya uhuru wa utendaji kazi wa waandishi katika
kuuhabarisha umma wa watanzania juu ya mambo yaliyokuwa yakitokea.
“Jeshi la Polisi
limekuwa na kawaida ya kuwanyanyasa, kuwapiga na hata kuwaua waandishi wa
habari pale wanapotekeleza wajibu wao wa kukusanya habari, ni vizuri sasa
serikali yetu ijirekebishe ione inakosea wapi”, alisema Rashid.
Hata hivyo ukatili
wa askari wa jeshi hilo kwa waandishi wa habari inakumbukwa zaidi pale
walipofanya mauaji ya Mwandishi wa kituo cha Televisheni ya Chanel ten mkoani
Iringa, Daud Mwangosi yaliyotokea Septemba 2 mwaka juzi, katika kijiji cha
Nyololo Mufindi mkoani humo wakati mwandishi huyo akiwajibika katika majukumu
yake ya kazi za kila siku.
No comments:
Post a Comment