Na
Kassian Nyandindi,
Mbinga.
MKUU
wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Senyi Ngaga amewashukia wafanyabishara wenye
tabia ya kutorosha kahawa wilayani humo kwa lengo la kukwepa kulipa ushuru na
kuwataka kuacha tabia hiyo mara moja, na atakaye endelea kufanya hivyo pale atakapobainika
atachukuliwa hatua kali za kisheria ikiwemo kunyang’anywa kibali cha ununuzi wa
zao hilo wilayani
humo.
Alitoa
onyo hilo wakati alipokuwa akifunga kikao cha
wadau wa kahawa kanda ya Ruvuma, kilichofanyika
katika ukumbi wa Jimbo Katoliki mjini hapa.
Ngaga
alisema haiwezekani kwa watu wachache hupenda kujinufaisha wao pekee kwa njia
zisizo halali kwa kutotaka kufuata taratibu zilizowekwa, ambapo dhamira ya
serikali ni kuona wananchi wake wananufaika kwa pamoja hivyo wilaya itaendelea
kusimamia hilo kwa nguvu zote kuhakikisha kwamba
hakuna mtu anayeweza kuhujumu biashara ya zao hilo.
Alifafanua
kuwa usambazaji wa mitambo ya kukoboa kahawa mbivu itaendelea kufanyika katika
maeneo mbalimbali yanayozalisha kahawa wilayani Mbinga, ikiwa ni lengo la kuona
wakulima wanafanikiwa kuzalisha kahawa yenye ubora na ambayo itapata bei nzuri
sokoni.
Alisema
kila mfanyabiashara anapaswa kufuata taratibu zilizowekwa katika ununuzi wa
kahawa kutoka kwa wakulima, ikiwemo matumizi ya vipimo sahihi ambavyo
haviwaibii wakulima.
Katika
hatua nyingine mkuu huyo wa wilaya, aliwataka wakulima na wafanyabiashara
kuacha tabia ya kuanika kahawa chini badala yake watumie vichanja ili kuweza
kutunza ubora wake usiharibike.
No comments:
Post a Comment