Na Kassian Nyandindi,
Songea.
WATU watatu wamefariki dunia na wengine 25
wamejeruhiwa vibaya baada ya basi walilokuwa wakisafiria kutoka Songea mjini mkoani Ruvuma, kwenda
jijini Mbeya kumgonga mwendesha baiskeli na baadaye kupinduka.
Habari zilizopatikana leo mjini hapa ambazo zimethibitishwa na Kamanda
wa polisi mkoani Ruvuma, Mihayo Msikhela amesema kuwa tukio hilo limetokea majira
ya saa 4:45 asubuhi, katika eneo la Sanangula nje kidogo ya Manispaa ya songea
mkoani humo.
Kamanda Msikhela amefafanua kuwa ajali hiyo imetokea kwenye
barabara ya kutoka Songea kwenda Njombe, ambapo namba za gari yenye usajili
T273 CDD aina ya Mitsubishi Rosa mali ya kampuni ya Super feo mjini Songea
ambalo lilikuwa linatoka Songea kwenda Mbeya.
Ameeleza kuwa basi hilo lilikuwa kwenye mwendo kasi ambapo mbele
yake kulikuwa na mwendesha baiskeli, hivyo dereva wa gari hilo aliyejulikana
kwa jina la Steven Mbigi (45) baada ya kumkwepa mwendesha baiskeli huyo na
kugonga mti na kupinduka kisha kusababisha watu wawili kufariki dunia papo hapo.
Alisema kuwa mwendesha baiskeli licha ya kujaribu kumkwepa,
alijeruhiwa vibaya hivyo pamoja na majeruhi wengine wamekimbizwa katika
hospitali ya mkoa huo kwa matibabu, ambako alifariki dunia akiwa chumba cha
mahututi wakati madaktari wakiendelea kumpa matibabu.
Kamanda Msikhela alisema kuwa maiti ya watu wawili pamoja na
majeruhi 24 bado hayajafahamika majina yao, lakini maiti zote mbili zimehifadhiwa
katika chumba cha kuhifadhia maiti kilichopo hospitali ya mkoa mjini Songea.
Pamoja na mambo mengine alieleza kuwa majeruhi wote majina yao bado
hayajatambulika na kwamba wamelazwa katika hospitali hiyo ambako wanaendelea
kupata matibabu.
Msikhela alisema chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi ambapo dereva aliyekuwa akiendesha gari hilo,
anadaiwa kutokomea kusikojulikana mara
tu baada ya ajali hiyo kutokea na Polisi
inaendelea kumsaka.
Kwa upande wake Mganga mfawidhi wa Hospitali ya mkoa Dokta
Benedict Ngaiza amethibitisha kupokea majeruhi 25 ambao mmoja kati ya majeruhi
hao aliyejulikana kwa jina la Aron Edward ambaye alikuwa amelazwa katika chumba
cha uangalizi maalum (ICU) alifariki dunia wakati akiendelea kupata matibabu.
No comments:
Post a Comment