Na Kassian Nyandindi,
Songea.
MWENYEKITI wa chama kikuu cha ushirika (SONAMCU) wilaya
Namtumbo mkoani Ruvuma, amefikishwa katika Mahakama ya mkoa huo akiwemo na Katibu
tawala msaidizi wa mkoa huo ambaye pia ni afisa ushirika wa mkoa huo, kwa
tuhuma za kula njama, kugushi nyaraka na kuiba fedha shilingi milioni 889.
Imedaiwa mahakamani hapo na mwanasheria wa serikali
Hamimu Mkoleye mbele ya Hakimu mkazi mfawidhi wa Mahakama ya mkoa huo Joackimu
Tiganga washtakiwa hao wote wawili wanalinganishwa na washitakiwa wengine 14
ambao walikwisha somewa mashitaka na kufanya idadi yao kuwa 16 ambapo wanadaiwa
kuiba fedha hizo.
Mkoleye amewataja waliofikishwa
mahakamani hapo kuwa ni Ally Athumani Bango (45) Mwenyekiti wa chama kikuu cha
ushirika Namtumbo (SONAMCO) ambacho kinajishughulisha na ununuzi wa zao la
tumbaku.
Mwingine ni Watson Nganiwa (57) Katibu
tawala msaidizi ofisi ya mkuu wa mkoa wa Ruvuma, ambaye pia ni Afisa ushirika wa
mkoa huo.
Amesema kuwa washitakiwa hao wanakabiliwa
na makosa mawili ya kula njama na kugushi nyaraka kisha kufanikiwa kuiba shilingi
milioni 889 mali ya vyama vya ushirika.
Kosa hili walilifanya kati ya mwaka 2011-2012
hadi 2013 na kwenda benki kuiba fedha hizo za wakulima.
Washitakiwa wote kwa pamoja wamekana
mashitaka na mmoja yuko nje kwa dhamana ambapo Ally Athumani ambaye ni Mwenyekiti
wa chama kikuu cha ushirika SONAMCO anaendelea kusota mahabusu baada ya kukosa
wadhamini wawili wenye sifa hivyo shauri hilo litatajwa tena Oktoba 9 mwaka huu.
No comments:
Post a Comment