Gari hilo lililopata
ajali likionekana katika picha tofauti likiwa limetumbukia katika korongo kijiji
cha Burma kata ya Nyoni wilayani Mbinga, baada ya dereva kuikosa kona kali
wakati alipokuwa kwenye mwendo kasi. (Picha zote na Kassian Nyandindi)
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
WATU sita ambao ni abiria waliokuwa wakisafiri kwa basi
kutoka Mbinga mjini kwenda makao makuu ya wilaya mpya ya Nyasa, mkoani Ruvuma
wamefariki dunia na wengine 18 kujeruhiwa vibaya baada ya gari hilo walilokuwa
wamepanda, kuacha njia na kutumbukia kwenye korongo.
Akizungumza na Mwandishi wa habari hizi, Kamanda wa Polisi wa
mkoa huo Mihayo Msikhela, alisema gari hilo lenye namba za usajili T 759 BVR aina ya Nissan
Civillian mali ya mfanyabiashara mmoja maarufu mjini hapa (jina halijapatikana) lilipata ajali Agosti Mosi mwaka huu, majira ya saa 10:30 jioni
katika kijiji cha Burma kata ya Nyoni wilayani Mbinga.
Mihayo alifafanua kuwa ajali hiyo ilisababishwa na gari kuwa
katika mwendo kasi, ambapo dereva aliyekuwa akiliendesha alishindwa kulimudu kwenye
kona kali na hatimaye lilitumbukia katika shimo kubwa (korongo) na kusababisha
mauaji na majeruhi hao.
“Mpaka sasa dereva aliyekuwa akiliendesha gari hili bado jina
lake halifahamiki kutokana na kukimbia kusikojulikana, Jeshi la polisi
tunafanya jitihada ya kumtafuta ili aweze kupatikana na baadaye tupate maelezo
yakinifu juu ya tukio hili”, alisema Mihayo.
Aliwataja walimu wa shule ya msingi waliofariki dunia kuwa ni
Esther Kumburu wa shule Kilimani wilayani Mbinga na Efigenia Kayombe ambaye ni mwalimu
wa shule ya Linda iliyopo Mbambabay wilayani Nyasa.
Vilevile kulikuwa na Ernest Ndunguru mkazi wa kijiji cha
Mikalanga wilayani Mbinga, Anna Chitete kijiji cha Kilosa wilayani Nyasa na
mmoja ambaye alifahamika kwa jina moja la Mbunda mkazi wa kitongoji cha Lusonga
Mbinga mjini, na kwamba maiti moja ambaye ni wa kiume bado hajatambuliwa jina
lake mpaka sasa.
Aidha Kamanda Mihayo alieleza kuwa maiti zote zimehifadhiwa
katika hospitali ya wilaya ya Mbinga, na kwamba majeruhi bado wanaendelea
kupatiwa matibabu katika hospitali hiyo lakini hali zao bado ni mbaya.
Hata hivyo alitoa wito kwa madereva wote mkoani Ruvuma,
kuacha kuendesha vyombo vya moto barabarani kwa mwendo kasi, ikiwemo vile ambavyo
vimekuwa vikibeba abiria kwani kufanya hivyo kuna hatarisha maisha ya watu
wanaosafiri, kutoka sehemu moja kwenda nyingine.
|
No comments:
Post a Comment