Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
MKUU
wa mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu amemuagiza Mkaguzi wa ndani wa
Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani humo kuhakikisha kwamba, anatoa
taarifa sahihi na kwa wakati juu ya mwenendo wa matumizi ya fedha za
miradi ya maendeleo ya wananchi wilayani humo ili kuepukana na
malalamiko yasiyokuwa ya lazima.
Sambamba
na hilo aliwataka watendaji husika katika halmashauri hiyo kutoingilia
utendaji kazi wa ofisi ya mkaguzi huyo, huku akisema kuwa ni ofisi
ambayo ipo huru na inafanya kazi zake bila kuingiliwa na mtu yeyote.
"Sasa
hivi ndugu zangu nahitaji mtambue kuwa ofisi ya mkaguzi wa ndani katika
halmashauri ni idara kamilifu ambayo ipo huru, kwa hiyo ninachosema
hapa mkaguzi fanya kazi zako bila kuingiliwa na
mtu wewe una jukumu kubwa sana", alisema Mwambungu.
Mwambungu
alitoa rai hiyo alipokuwa akihutubia leo kwenye kikao cha Baraza
la Madiwani la Halmashauri ya wilaya Mbinga, lililofanyika kwenye
ukumbi wa jumba la Maendeleo uliopo mjini hapa.
Aidha
Mwambungu aliwataka Madiwani wa wilaya hiyo kusimamia kikamilifu fedha
za miradi ya maendeleo ya wananchi, kwa kuhakikisha kuwa miradi ya
wananchi inajengwa kwa viwango vinavyokubalika. (Value for money)
Mkuu
huyo wa mkoa alisisitiza kuwa mtendaji yeyote ndani ya halmashauri hiyo
atakayeonekana anakikuka taratibu za utumishi wa umma kwa lengo la
kujinufaisha yeye binafsi, atachukuliwa hatua za kisheria ili iwe
fundisho kwa wengine.
"Lazima
muwe makini sana katika kazi zenu, muitendee haki nafasi mliyonayo,
Madiwani simamieni majukumu yenu ya kazi ipasavyo katika kata zenu",
alisisitiza.
Hata
hivyo aliongeza kuwa ni muhimu kwa
fedha zinazokusanywa kupitia ushuru wa aina mbalimbali, zirudi vijijini
kwa wananchi katika kutekeleza miradi husika na sio kuishia mifukoni
kwa wajanja wachache wenye nia mbaya ya kurudisha nyuma maendeleo ya
wananchi.
No comments:
Post a Comment