Na Kassian Nyandindi,
Ruvuma.
NAIBU Waziri wa elimu na mafunzo ya ufundi, Jenister Mhagama
ameipongeza wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma kuwa ya kwanza kitaifa kufanya
vizuri kielimu kwa shule za msingi, katika maendeleo ya mpango wa kipimo cha matokeo
makubwa hapa nchini (BRN).
Mhagama alitoa pongezi hizo wakati alipokuwa akizungumza na
wakazi wa mji wa Mbinga, na kusema kuwa matokeo hayo yametokana na viongozi wa
wilaya hiyo kushirikiana ipasavyo na walimu katika kutekeleza majukumu yao ya
kazi.
“Wilaya hii ya Mbinga imekuwa mstari wa mbele katika
kujitolea kuboresha maendeleo kwenye sekta ya elimu, nawapongeza sana nawaomba
endelezeni jitihada hizi kwa faida ya kizazi chetu cha sasa na baadae”, alisema
Mhagama.
Waziri huyo alieleza kuwa serikali katika bajeti ya fedha
mwaka huu, imetenga shilingi bilioni 43 kwa ajili ya kuboresha kitengo cha
ukaguzi hapa nchini ili kiweze kuendelea kufanya kazi zake za ukaguzi kwa
ufasaha kwa shule za msingi na sekondari.
Vilevile aliongeza kuwa kwa wilaya ya Mbinga shilingi milioni
176 shule za sekondari wilayani humo zimepewa kwa ajili ya kuboresha
miundombinu husika.
Hata hivyo alitolea ufafanuzi juu ya tatizo la upungufu wa
walimu wa masomo ya sayansi wilayani hapa, kwamba serikali inalifanyia kazi na
watakapopatikana wakati wowote itawaleta ili kuweza kumaliza changamoto hiyo.
No comments:
Post a Comment