Baadhi ya Washiriki wakifuatilia mada zilizokuwa zikitolewa na wakufunzi wa mafunzo hayo. (Picha zote na Kassian Nyandindi) |
Na Kassian
Nyandindi,
Mbinga.
IMESISITIZWA kuwa mama mjamzito anatakiwa kwenda kliniki
mapema mara baada ya kujitambua kuwa ni mjamzito, ili aweze kujifungua salama
na kuepukana na madhara yanayoweza kutokea baadae.
Aidha katika kuleta ufanisi Wahudumu wa afya wilaya ya Mbinga
na Nyasa mkoani Ruvuma, wametakiwa kuhamasisha jamii kuona umuhimu wa utekelezaji
wa jambo hilo kwa lengo la kuachana na vitendo vya akina mama wajawazito kujifungulia
majumbani, badala yake waende kwenye vituo vya afya, zahanati au hospitali.
Rai hiyo ilitolewa leo na Mratibu wa mfuko wa afya ya jamii
(CHF) wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, Alphonce Njawa alipokuwa akifungua mafunzo
ya siku mbili kwa wahudumu wa afya watendaji wa vijiji wa wilaya hizo, ambayo yamendaliwa
na shirika lisilo la kiserikali ‘Tanzania Communication and Development Center’
(TCDC) yaliyofanyika katika ukumbi wa Jumba la maendeleo mjini hapa.
Njawa alisema kuwa mafunzo hayo yameandaliwa kwa lengo la
kuwapa taarifa za mabadiliko ya kiutendaji na ongezeko la maeneo ya kufanyia kazi,
pamoja na kutoa elimu ya afya kwenye jamii kuepukana na tabia hiyo na hatimaye hata
kupunguza vifo visivyo vya lazima.
“Ndugu zangu mafunzo haya yanalenga pia huko tuendako
tujitahidi kuhamasisha wananchi vijijini kuachana na mitandao ya ngono ambayo
kwa kiasi kikubwa imekuwa ikieneza kwa kasi maambukizi ya virusi vya ugonjwa wa
ukimwi”, alisema.
Alisema Wahudumu hao hawana budi kuzingatia maagizo
watakayopewa, ambayo yataleta mabadiliko chanya katika jamii na hatimaye kuweza
kufikia malengo ya kupunguza tatizo la maambukizi ya ugonjwa huo.
Kwa upande wake Meneja wa mkoa wa Ruvuma wa TCDC Assely
Mwamaka alisema shirika hilo limekuwa likijikita katika shughuli zake kwenye
maeneo matatu ambayo ni kutokomeza ugonjwa wa malaria, kuongeza matumizi ya uzazi
wa mpango na kuzuia maambukizi mapya ya virusi vya ukimwi.
Mwamaka alieleza kuwa maeneo hayo yanalenga kutatua matatizo
ya msingi kuhusu afya ya jamii, ambayo yameendelea kuwa mzigo mkubwa kwa
familia au kaya hapa nchini.
Vilevile aliwataka Wahudumu hao wa afya huko vijijini waende
kuelimisha wazazi wenye vyandarua vya ziada wawapatie wenzao ambao hawana
vyandarua, na sio kubaki navyo majumbani mpaka kufikia hatua ya kuharibika au
kufanyia matumizi ambayo sio sahihi.
Alisema baadhi ya maeneo hapa mkoani Ruvuma, kumekuwa na tabia
ya watu kutumia vyandarua kwa matumizi ambayo sio sahihi kama vile kuzungushia
uzio wa bustani au kufanyia shughuli za uvuvi wa dagaa, katika maeneo ya
mwambao mwa ziwa Nyasa jambo ambalo ni kinyume na taratibu zilizowekwa.
Kufuatia hali hiyo Meneja huyo aliwaagiza watendaji wa kata
kuwachukulia hatua watu wanaofanya hivyo, ili kuweza kudhibiti vitendo hivyo
ambavyo havileti picha nzuri katika jamii.
No comments:
Post a Comment