Thursday, July 17, 2014

KITUO CHA POLISI TUNDURU CHAVAMIWA NA KUVURUGWA



Na Mwandishi wetu,
Songea.
JESHI la Polisi mkoani Ruvuma linaendesha msako mkali katika kijiji cha Lukumbule wilayani Tunduru mkoani humo, kwa lengo la kuwapata wahuni waliovamia kituo cha Polisi kung’oa bati, kuiba sola na kuchoma pikipiki ya askari wa usalama barabarani.
Kamanda wa Polisi wa mkoa huo Mihayo Msikela akizungumza na Waandishi wa habari mjini hapa alisema tukio hilo lilitokea Julai 11 mwaka huu, majira ya asubuhi wakati askari wa usalama barabarani mwenye namba H 925  Benjamini, akiwa na askari mwenye namba G 1921 Charles walipomsimamisha Sijaona Ally ambaye hakutii amri hiyo badala yake kumgonga askari wa usalama barabarani.
Kamanda Msikela amesema kutokana na wote wawili kupata majeraha walikimbizwa hospitali ya Lukumbule kwa matibabu zaidi.
Wananchi baada ya kusikia askari wa usalama barabarani yuko katika hospitali ya Lukumbule waliandamana na kutaka askari Benjamini atolewe mara moja asitibiwe hapo.
Kamanda Mihayo alisema wananchi hao hawakuishia hapo walienda kituo cha polisi cha Lukumbule na kung’oa bati, kuiba sola pamoja na kuchoma moto pikipiki ya askari Benjamin.
Kufuatia tukio hilo Kamanda huyo wa polisi amewataka wananchi kuachana na vitendo vya uchukuaji wa sheria mkononi.
 

No comments: