Rais Jakaya Kikwete akiangalia vikundi vya ngoma katika kituo kikuu cha Mabasi mjini Mbinga, mara baada ya kuwasili akitokea wilaya ya Nyasa. Upande wa kulia ni Mkuu wa wilaya hiyo Senyi Ngaga. |
Mbinga.
RAIS wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Jakaya Kikwete
amewataka wakulima wanaozalisha zao la kahawa wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, kutumia
fedha walizokopeshwa na shirika la hifadhi ya jamii (NSSF) kwa makusudio
yaliyowekwa na sio vinginevyo.
Kikwete alisema hayo baada ya kukabidhi hundi ya shilingi
bilioni 2 kwa vyama vinne vya ushirika ambavyo hujishughulisha na uzalishaji wa
zao hilo wilayani humo, ambavyo kila kimoja vimekopeshwa shilingi milioni 500.
Aliwataka viongozi na wanachama wa ushirika husika, kuwa na
nidhamu katika matumizi ya fedha hizo ili waweze kurejesha kwa wakati na wanachama
waweze kunufaika na mkopo huo.
Awali akisoma taarifa ya NSSF juu ya mpango wa kuwafikia
wakulima wote wa wilaya hiyo, Kaimu Mkurugenzi wa shirika hilo Chiku Matessa
alisema wazo la kuanzisha mpango huo ni msukumo uliotokana na changamoto
wanazokabiliana nazo wakulima katika kuendeleza kilimo kutoka na kukosa fedha.
Matessa alieleza kwamba baada ya kuona hilo, shirika liliona
ni vyema lianze kutoa mikopo kwa wakulima wadogo wadogo yenye gharama nafuu ili
waweze kuondokana na adha hiyo
wanayoipata sasa, hatimaye waweze kujikwamua kiuchumi na kuondokana na lindi la
umasikini.
Alisema changamoto hizo ni pamoja na kukosa uhakika wa huduma
za afya, kutokuwa na uwezo wa kununua pembejeo ili kuongeza uzalishaji na
uhakika wa kipato baada ya kufikia umri wa uzee ambapo husababisha kushindwa
kuendelea na shughuli za kilimo.
Mkurugenzi huyo alivitaja vyama vinne vya ushirika wilayani
Mbinga ambavyo vilipatiwa mkopo huo ni Mahilo, Ngaka, Ngima na Pilikano.
Hata hivyo alisema shirika linatoa wito kwa wakulima wote wa
wilaya hiyo ambao hawajajiunga na vyama vya ushirika wajiunge, na NSSF ili
waweze kunufaika na mafao ikiwemo hata na mikopo yenye riba nafuu.
No comments:
Post a Comment