Na Kassian Nyandindi,
Songea.
RAIS Jakaya Kikwete amesema serikali imetenga shilingi bilioni 15
zikazotumika kununulia mazao ya wakulima, kupitia wakala wa hifadhi ya chakula
ya taifa nchini(NFRA) kuanzia Agosti mosi mwaka huu msimu wa mavuno ya zao la mahindi
utakapofunguliwa.
Akizungumza mara baada ya kukagua na kuzindua ghala jipya la
hifadhi ya taifa ya chakula, lililopo eneo la Ruhuwiko mjini Songea alisema
kuwa ili kuweza kuhifadhi mazao mengi kwa wakati mmoja ni lazima pawe na
maghala mengi na ya kisasa.
Alisema hivi sasa taifa lina akiba ya kutosha ya chakula ambapo
maghala yake yamejaa mazao, ikiwemo ghala la NFRA la mjini hapa ambapo kuna
tani 51,000 ambazo bado hazijaondolewa huku wakati wa kununua mazao mapya ukiwa
umewadia.
Kikwete alisema kuwa mpango unaendelea kufanyika ili mahindi
yaliyopo yaweze kuuzwa katika nchi ambazo zina upungufu mkubwa wa chakula
ikiwemo Kenya,Sudan Kusini na shirika la WFP ambapo kwa kufanya hivyo maghala
yaliyofura mazao yatakuwa wazi na kuweza kupata nafasi ya kuweka mazao
yatakayonunuliwa.
Alisema serikali itaendelea kuiwezesha NFRA ili iweze kununua
mazao ya wakulima jambo ambalo litasaidia kuwapatia bei nzur, na hivyo
kuepukana na wafanyabiashara walanguzi ambao siku zote wamekuwa na kawaida ya
kuwaibia kutokana na kununua mazao yao kwa bei ya chini.
Rais aliwataka wakulima kutokuwa na haraka ya kuuza mazao yao kwa
walanguzi hao, badala yake wasubiri msimu ufunguliwe na kwamba alisisitiza juu
ya umuhimu wa kujiunga pamoja na kuanzisha vikundi vya ujasiriamali jambo
ambalo pia litapelekea wauze mazao yao kwa pamoja.
Awali katika taarifa yake Naibu waziri wa kilimo na chakula
Godfrey Zambi alisema NFRA inahitaji kiasi cha shilingi bilioni 211, kwa ajili
ya ujenzi wa maghala ya kuhifadhia mazao ya chakula na kwamba mpaka sasa kuna
maghala 31 nchini kote.
Zambi alisema kuwa lengo la serikali ni kununua tani 400,000
ifikapo mwaka 2016/17 hivyo ili kufanikisha zoezi hilo, jitihada kubwa
zinapaswa kufanyika kufanikisha ujenzi wa maghala hayo ambayo yatatumika
kuhifadhia mazao baada ya kununua kutoka kwa wakulima.
Wakati huohuo Rais Jakaya Kikwete amesema rushwa imeshamiri katika
kitengo cha manunuzi jambo ambalo limekuwa likisababisha miradi mingi ya
kimaendeleo ishindwe kukamilika kwa viwango vinavyotakiwa, na kuiagiza taasisi
ya kuzuia na kupambana na rushwa(TAKUKURU)ihakikishe inafuatilia kwa umakini
eneo hilo.
Akizungumza mara baada ya kufungua ofisi ya TAKUKURU mkoani Ruvuma
iliyojengwa kwa gharama ya shilingi bilioni 1.1 alisema matumizi mabaya ya
madaraka na fedha za umma zinazoelekezwa kwenye miradi ya maendeleo, haiwezi
kufumbiwa macho hivyo jitihada za makusudi zinapaswa kufanyika ili kukabiliana
na wale wote wenye tabia hiyo inayorudisha nyuma jitihada za serikali za
kuwaletea wananchi maendeleo.
Kikwete alisema kuwa serikali inathamini kazi kubwa zinazofanywa
na TAKUKURU hivyo itaendelea kuwajengea uwezo ili waweze kupata mafanikio
makubwa, katika utendaji wao na kwamba elimu kwa umma ni muhimu kuendelea
kutolewa jambo ambalo litaifanya jamii kuweza kutoa ushirikiano kwao.
Aliiasa taasisi hiyo kutokubali kunyooshewa kidole na wananchi kwa
kuchelewa kuchukua hatua katika maeneo yale ambayo wanakuwa wamepata taarifa
ihisuyo matumizi mabaya ya fedha za serikali, na kwamba katika kuhakikisha kazi
yao inakuwa rahisi serikali itahakikisha inaongeza idadi ya watumishi,vitendea
kazi na kuendelea kujenga ofisi tatu kila mwaka.
Katika hatua nyingine Rais Kikwete amefungua mradi wa nyumba za
gharama nafuu mjini hapa ambazo zimejengwa na shirika la nyumba za taifa(NHC)
ambapo zimejengwa nyumba 18 ambazo mpaka kukamilika kwake zitagharimu shilingi
milioni 676.2
Aliwaleleza wananchi mara baada ya kufungua nyumba hizo Rais
alizitaka halmashauri za wilaya na manispaa kote nchini kuhakikisha zinatenga
maeneo ambayo shirika hilo litajenga nyumba hizo za gharama nafuu, na kwamba
pindi zinapokamilika wananchi wakope fedha katika taasisi za fedha na kununua
nyumba hizo ambazo kimsingi zimelenga kuwasaidia wananchi wenye kipata cha
chini.
Alilipongeza shirika la nyumba la taifa kwa kuona umuhimu wa
kusaidia juhudi za serikali za kutoa ajira kwa vijana kutokana na kitendo chake
cha vijana katika halmashauri za wilaya kote nchini kusaidiwa mashine kwa ajili
ya kufyatua matofari na kuyauza.
Kikwete alisema utaratibu huo licha ya kuongeza ajira kwa vijana
pia utasaidia kubadili sura ya miji kutokana na ukweli kwamba, hakutakuwa na
tatizo la upatikanaji wa matofari ya kujengea nyumba za kisasa.
No comments:
Post a Comment