Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dokta Jakaya Kikwete. |
Na Kassian
Nyandindi,
Ruvuma.
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dokta Jakaya Mrisho Kikwete atafanya ziara ya
kikazi mkoani Ruvuma ikiwemo kukagua, kufanya uzinduzi na kuweka mawe ya msingi
katika miradi mbalimbali ya Wananchi mkoani humo.
Ziara hiyo ni ya muda wa siku saba anatarajia kuwasili katika
uwanja wa ndege mjini Songea Julai 17 mwaka huu, majira ya saa tano asubuhi na
kupokelewa na uongozi wa mkoa huo.
Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu ametoa taarifa hiyo leo
kwa vyombo mbalimbali vya habari, alipokuwa akizungumza na Waandishi wa habari
mjini hapa kwenye ukumbi wa Maliasili wa mkoa huo.
Mwambungu amewataka wananchi waliopo katika maeneo mbalimbali
mkoani humo, ambako Rais Kikwete atapita kufanya shughuli hizo muhimu ikiwemo mikutano
ya hadhara katika kila wilaya zilizopo hapa mkoani
Ruvuma, kujitokeza kwa wingi.
Alisema Rais Kikwete akiwa katika Manispaa ya Songea ataweka
jiwe la msingi nyumba bora za gharama nafuu ambazo zimejengwa na shirika la
nyumba la Taifa (NHC), Ofisi ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU)
ya mkoa wa Ruvuma.
Kadhalika ataendelea na shughuli za ukaguzi na uzinduzi wa ghala
jipya la hifadhi ya Taifa ya chakula (NFRA) lililopo mjini Songea, daraja jipya
la Ruhekei na mradi wa umeme vijijini (REA) uliopo Mbamba bay wilayani Nyasa.
Pia atafanya ufunguzi wa barabara kuu ambayo imejengwa kwa
kiwango cha lami ya kutoka Mbinga hadi Songea na kituo kikuu cha mabasi ambacho
kimejengwa Mbinga mjini.
Rais Kikwete wakati atakapokuwa akiendelea na ziara yake mkoani
Ruvuma, atafungua soko la kimataifa la Mkenda ambalo limejengwa mpakani mwa
nchi ya Tanzania na Msumbiji ambalo litawanufaisha wananchi wa pande hizo
mbili.
Wilayani Namtumbo atafanya uzinduzi wa hospitali ya wilaya
hiyo, barabara iliyojengwa kwa kiwango cha lami kutoka Songea hadi Namtumbo.
Uzinduzi rasmi wa ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kutoka
Namtumbo, Tunduru hadi Sauti moja wilayani Tunduru.
Wilayani Tunduru ataendelea na uzinduzi wa nyumba 40 ambazo
zimejengwa na taasisi ya Mkapa foundation zilizopo katika kijiji cha Matemanga
na mradi wa maji uliopo tarafa ya Nalasi wilayani humo.
Hata hivyo Rais Kikwete atahitimisha ziara yake Julai 23
mwaka huu, kwa kufanya majumuisho Tunduru mjini na kuondoka wilayani humo
kwenda Nachingwea kuelekea Jijini Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment