Na Dustan Ndunguru,
Mbinga.
BALOZI wa China nchini Lu
Youqing amempongeza Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Dokta Jakaya
Kikwete kutokana na kazi yake kubwa, anayoifanya ya kusimamia shughuli za
ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami jambo ambalo litasaidia kurahisisha
upatikanaji wa maendeleo.
Pongezi hizo alizitoa
wakati alipokuwa akiongea katika mkutano wa hadhara mjini hapa, mara baada ya
Rais Kikwete kufungua rasmi barabara ya lami kutoka Mbinga hadi Peramiho yenye
urefu wa kilometa 78 ambayo imejengwa na kampuni ya SINOHYDRO ya nchini China.
Lu Youqing alisema kuwa
watanzania wanapaswa kuendelea kuunga jitihada zinazofanywa na serikali yao,
ili waweze kuondokana na umasikini wa kipato na kwamba serikali ya China
itaendelea kushirikiana na Tanzania katika masuala mbalimbali ya kimaendeleo.
Alisema kama nchi nataka
kupata uchumi mzuri ni lazima kujenga barabara kwa kiwango kinachoridhisha kazi
ambayo Tanzania imekuwa ikilitekeleza kwa manufaa ya wananchi wake, na kwamba
ushahidi upo wazi kutokana na kila kona kuwepo kwa wakandarasi wanaoshughulikia
ujenzi wa miundombinu ya barabara.
Balozi huyo alisema
kwa kutumia barabara hizo wananchi wataweza kuuza mazao yao sokoni
kiurahisi na hivyo kujikwamua kiuchumi na kwamba aliwaasa wananchi, kuepuka
vitendo vya wizi katika barabara hiyo kwani kwa kufanya hivyo barabara
itaharibika mapema.
Naye Waziri wa ujenzi John
Magufuli alisema Rais Kikwete ataendelea kukumbukwa kutokana na juhudi zake za
kutekeleza kwa vitendo ahadi zake alizozitoa kwa wananchi katika maeneo
mbalimbali hapa nchini, ambapo moja ya ahadi ambayo aliitoa ni ya ujenzi wa
barabara ya Mbinga hadi Peramiho kwa kiwango cha lami ahadi ambayo imekamilika.
Magufuli alisema Wizara
yake imekuwa ikitekeleza kwa vitendo yale yote ambayo yanaelekezwa na serikal,
hivyo wananchi kwa upande wao nao hawana budi kuendelea kuunga mkono juhudi
hizo za kuwaletea maendeleo ili hatimaye lengo la kuondokana na umasikini
liweze kupata mafanikio yaliyokusudiwa.
No comments:
Post a Comment