Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
IMEELEZWA kuwa asilimia 95 ya ardhi wilayani Mbinga mkoa wa
Ruvuma, inamilikiwa na wanaume wakati asilimia tano tu ndio humiliki wanawake wachache huku mila na desturi zikiwakandamiza wanawake na kuwanyima
fursa, ya kumiliki rasilimali hiyo muhimu.
Sambamba na hilo wanawake sita kati ya 10 wilayani humo ndio
ambao huporwa ardhi za mashamba yao na ndugu wa marehemu baada ya kufiwa na
mume, hivyo katika kuondokana na tatizo hilo jitihada za makusudi zinapaswa
kuchukuliwa ili kuweza kuondokana na hali hiyo.
Kufuatia hali hiyo, umoja wa kikundi cha maendeleo ya wanawake
(KIUNGI) wilayani Mbinga umeweza kutambua matatizo hayo yanayowakabili wanawake
wilayani humo, katika dhana nzima ya umiliki wa rasilimali ardhi na kuanza kutoa
elimu juu ya haki za kundi hilo kumiliki ardhi.
Katika kuharakisha mafanikio ya utekelezaji wa suala hilo, Cecilia
Mbata ambaye ni Ofisa ustawi maendeleo ya jamii kitengo cha wanawake wilayani
humo, alisema mafunzo ya siku tatu yametolewa ambayo yamefadhiliwa na shirika lisilo la kiserikali 'The foundation for civil Society', yalishirikisha pia wanaume
ili wasiwe pingamizi badala yake wahamasishe jamii ya wanambinga juu ya haki ya
mwanamke katika kumiliki rasilimali hiyo.
Alisema kuwa KIUNGI imeweza kutoa mafunzo hayo kwa kuanzia
kata mbili za Litembo na Linda wilaya ya Mbinga, ambapo wanawake na wanaume wameweza
kuelimishwa na kutambua haki zao za kumiliki ardhi, na sio kuendesha malumbano
katika jamii yasiyokuwa ya lazima.
Mbata alisema lengo la kufanya hivyo ni baada ya wanaumoja wa
kikundi hicho kutambua na kuona kwamba, wakati umefika sasa kwa mwanamke kujua
au kufahamu miongozo, sera na sheria mbalimbali zinazowagusa wanawake katika
kutetea mambo yao ya msingi.
Hivyo basi KIUNGI imetambua kuwa pamoja na serikali kuweka mikakati
hiyo, lakini walengwa bado hawajui na ndio maana hata utekelezaji wake umekuwa
mgumu hususan katika maeneo ya vijijini.
Pamoja na mambo mengine naye Meneja mkuu wa umoja huo Renatha
Kapinga, alifafanua kuwa elimu hiyo itaendelea kutolewa kwa wanawake wote wa
Mbinga ikiwa ni lengo la kuwafanya waweze kuondokana na mila na desturi
kandamizi katika kupata haki zao za msingi juu ya masuala ya kumiliki ardhi.
No comments:
Post a Comment