Na Kassian Nyandindi,
Namtumbo.
RAIS Jakaya Kikwete
amemuagiza Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu ahakikishe kwamba anawakamata
na kuwafikisha Mahakamani wale wote ambao wamehusika kwa namna moja au
nyingine, kufanya ubadhirifu wa fedha za wakulima wa tumbaku wilaya ya Songea
na Namtumbo mkoani humo.
Aidha agizo hilo
limefuatia baada ya Mwambungu kuunda tume ya kuchunguza tatizo hilo, ambayo
inaendelea kufanya kazi ya ukaguzi wa hesabu za fedha kwa chama cha ushirika wa
wakulima wanaozalisha zao hilo kutoka kwenye wilaya hizo mbili (SONAMCU).
Kikwete ambaye
alionekana kukerwa na kitendo hicho na kufikia hatua ya kutoa agizo hilo, baada
ya kupokea malalamiko kutoka kwa Mbunge wa Jimbo la Namtumbo Vita Kawawa,
katika mkutano wa hadhara wa wananchi uliofanyika mjini hapa.
Mbunge huyo alimnyoshea
kidole Mrajisi wa vyama vya ushirika mkoani Ruvuma Watson Nganiwa kwa
kushirikiana na maofisa ushirika wenzake, wanadaiwa kushiriki katika kufanya
ubadhirifu wa mamilioni ya fedha huku wakulima wa tumbaku wakiendelea kubaki
kuwa masikini.
Alisema licha ya tatizo
hilo kuonekana kuwa sugu kutokana na kudumu kwa miaka mingi sasa, imefikia
hatua wakulima wa zao hilo wamekatishwa tamaa kuendelea na kazi ya kilimo hicho
kutokana na fedha zao kuibwa mara kwa mara na wajanja wachache.
Kawawa alifafanua kuwa
ni jambo la kushangaza kwa mtumishi wa umma kuona anawaibia wakulima fedha zao,
wakati amepewa dhamana na serikali ya kuhakikisha anasimamia ipasavyo mali za
umma.
“Mheshimiwa Rais
viongozi wa ushirika ngazi ya mkoa wana matatizo wamekuwa wakiiba fedha za
wakulima hata hawaoni aibu, huku mkulima huyu akiendelea kuteseka kila siku kwa
jembe la mkono”, alisema.
Katika hatua nyingine
Rais Kikwete alisikitishwa pia na matokeo mabaya ya kumaliza elimu ya msingi na
sekondari wilayani Namtumbo, ambapo wilaya hiyo katika kipindi cha mwaka 2012
na 2013 imeendelea kufanya vibaya.
Matokeo mabaya ya ufaulu
watoto wa shule za msingi na sekondari katika wilaya hiyo, kunatokana na
kukithiri kwa tatizo la utoro na watoto wa kike kupewa mimba huku wahusika
kutochukuliwa hatua stahiki za kinidhamu ili kuweza kudhibiti hali hiyo.
Taarifa ya maendeleo ya
wilaya hiyo inasema kuwa wanafunzi 4509 waliomaliza darasa la saba mwaka 2013
walikatisha masomo yao kutokana na kuwa na ujauzito, huku wanafunzi 3015
wakishindwa kumaliza masomo yao kufuatia kuwepo kwa tatizo la kutohudhuria
masomo darasani (utoro).
Vilevile kwa upande wa
shule za sekondari kwa mwaka huo, wanafunzi 1742 hawakumaliza kidato cha nne
kutokana na tatizo la utoro huku 997 wakiwa na mimba.
No comments:
Post a Comment