Na Steven Augustino,
Tunduru.
HALMASHAURI ya wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma huenda ikapata
hati chafu katika mwaka huu wa fedha, kutokana na halmashauri hiyo kutotekeleza ipasavyo
ujenzi wa miradi 16 ya maendeleo ya wananchi kwa mwaka wa fedha wa 2013/2014
yenye thamani ya shilingi milioni 284.3.
Mwakilishi wa mkaguzi na mdhibiti wa hesabu za serikali mkoani Ruvuma, Leonard
Chama alisema kuwa tatizo hilo linatokana na halmashauri hiyo kushindwa kusimamia ipasavyo ujenzi wa zahanati, madarasa, visima vya maji na ofisi ya
kata.
Kufuatia hali hiyo Baraza la madiwani la halmashauri hiyo limesikitishwa
na hali hiyo na kuutaka uongozi husika wa wilaya ya Tunduru kuhakikisha kwamba
makosa hayo hayajirudii tena.
Hayo yalijiri katika kikao cha dharula cha baraza hilo
kilichoketi kwenye ukumbi wa Klasta ya walimu tarafa ya Mlingoti mjini hapa, baada
ya kutolewa kwa taarifa ya Mdhibiti na mkaguzi wa hesabu za serikali ambapo
ilionesha kuwa miradi ya maendeleo ya wananchi wilayani humo utekelezaji wake, umekuwa
ni wa chini ya kiwango na haukidhi mahitaji halisi.
Awali katika ufunguzi wa kikao hicho Mwanyekiti wa
Halmashauri ya wilaya ya Tunduru Faridu Khamisi, pamoja na mambo mengine aliwataka madiwani
hao kuchangia hoja zao bila uoga na kwamba lengo la kikao hicho ni kupitia na
kupitisha hoja hizo za mkaguzi.
Akiwasilisha taarifa ya kamati ya fedha, uongozi na mipango,
makamu Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, ambaye ni diwani wa kata ya Mchoteka Mkwanda
Sudi alisema kuwa taarifa hiyo ya mkaguzi na mdhibiti wa hesabu za serikali ilipitiwa na kudadavuliwa ipasavyo hatimaye kubaini
mapungufu yaliyopo.
Pia diwani wa kata ya Mlingoti Mashariki Ally Mchemela alielezea
juu ya mapungufu yaliyojitokeza, ambapo kulikuwepo ukiukwaji wa taratibu husika
kwa Kampuni State business Company Limited iliyopewa zabuni ya kukusanya
ushuru wa mazao baada ya kubainika kupoteza vitabu viwili vilivyokuwa
vikitumika kukusanyia mapato, kwa halmashauri ya Tunduru huku akiachwa huru
bila kuchukuliwa hatua za kisheria.
No comments:
Post a Comment