Na Kassian
Nyandindi,
Mbinga.
TAASISI ya Kuzuia, Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) wilayani
Mbinga mkoa wa Ruvuma imesema, wilaya hiyo inakabiliwa kwa kiasi kikubwa na
vitendo vya rushwa katika miradi ya maendeleo ya wananchi ikiwemo ujenzi wa
majengo ya shule, barabara na miradi mbalimbali ya kilimo.
Aidha rushwa kubwa imetawala hasa kwenye kitengo cha manunuzi,
ambapo jitihada zinaendelea kufanyika kuchunguza matatizo husika yaliyopo na
tayari baadhi ya vigogo wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga wamefikishwa
Mahakamani kujibu makosa yanayowakabili.
Hayo yalisemwa jana na Kamanda wa TAKUKURU wa wilaya hiyo
Ditram Mhoma alipokuwa akizungumza na Waandishi wa habari, ambao walitembelea
banda la taasisi hiyo la kuelimisha jamii namna ya kupambana na rushwa, katika
uwanja wa mkesha wa mbio za mwenge wa Uhuru kata ya Maguu wilayani humo.
Mhoma alifafanua kuwa viongozi sita wamefikishwa katika
Mahakama ya wilaya ya Mbinga, wakikabiliwa na tuhuma za matumizi mabaya ya
fedha za miradi ikiwemo ujenzi wa barabara na majengo ya kutolea huduma za
afya.
Alibainisha kuwa kuna baadhi ya miradi ambayo iligharimu
fedha nyingi imejengwa chini ya kiwango na kusababisha kufikia hatua ya
kubomoka.
Pamoja na mambo mengine alisema changamoto kubwa
wanayokabiliana nayo katika kuendesha kesi mahakamani, ni ushirikiano mdogo unaotolewa
kutoka kwa wananchi ambapo wengi wao wamekuwa hawataki kwenda kutoa ushahidi.
“Wakati tunapofanya uchunguzi wananchi wamekuwa wakitupatia
ushirikiano wa kutosha, lakini tunapofikia hatua ya kuendesha kesi mahakamani
hawataki kuja kutoa ushahidi, hii ndiyo changamoto kubwa tunayokabiliana nayo
na kuonekana kesi nyingi zinaishia mahakamani kwa watuhumiwa kutopatikana na
makosa hatimaye huachiwa huru bila kuchukuliwa hatua”, alisema.
Hata hivyo Mhoma aliiomba jamii kwa ujumla ishiriki
kikamilifu dhidi ya mapambano ya rushwa kwenye maeneo yao, hasa katika kutoa
ushahidi mahakamani pale wanapotakiwa ikiwemo pia wakemee vitendo hivyo hasa
kwenye maeneo yao ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya wananchi.
No comments:
Post a Comment