Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
VIFO vinayotokana na akina mama wajawazito wakati wa
kujifungua hapa nchini, vimepungua kutoka akina mama 578 miaka ya nyuma na
kufikia 454 mwaka huu kati ya vizazi hai 100,000 ambao walikuwa wakijifungulia nyumbani
na kusababisha mtoto au mama kufariki dunia.
Upungufu huo umetokana na jitihada ya serikali kufanya kazi
ya ujenzi wa zahanati vijijini na vituo vya afya kwa kila kata, ambapo akina
mama wengi wajawazito huenda huko kwa ajili ya kupata huduma husika tofauti na
kujifungulia majumbani.
Hayo yalisemwa leo na mke wa Rais hapa nchini, Mama Salma
Kikwete alipokuwa akizungumza na wananchi wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma.
Mama Salma alisema ujenzi wa vituo hivyo vya kutolea huduma
za afya vijijini ulilenga kupunguza tatizo hilo, na kwamba ni ahadi iliyotolewa
na Chama Cha Mapinduzi na ambayo ipo katika ilani yake.
“Ndugu zangu wanambinga ilani ya CCM imetekeleza ujenzi wa
zahanati na vituo vya afya, wakati huu sasa sio wakati tena wa mama mjamzito au
motto kupoteza maisha ni wakati wa kwenda kujifungulia huko ili tuepukane na
matizo yanayoweza kutokea baadaye”, alisema Mama Kikwete.
Aidha aliwataka akina mama hao kabla ya kujifungua wa wahi
kliniki mapema kupima afya zao, kwa lengo la kujitambua kama wana maambukizi ya
virusi vya Ukimwi au la ili waweze kufungua mtoto aliyesalama ambaye hana
maambukizi ya ugonjwa huo.
“Kujua afya ndio kujua usalama wako, nendeni kliniki mkapime
afya zenu ili kujua kama mna maambukizi lengo ni kumpata mtoto aliyekuwa salama”,
alisisitiza.
Pamoja na mambo mengine alisema baadhi ya akina mama
wanapojifungua hupatwa na tatizo la ugonjwa wa fistula ambapo hutokwa na mkojo
mfululizo, hivyo aliwataka wananchi wa mkoa wa Ruvuma endapo kama kuna mama wa
aina hiyo haraka apelekwe hospitali ili aweze kupatiwa matibabu kabla tatizo
kuwa kubwa.
Mama Salma alifafanua kuwa baadhi ya kaya zikiona mama ana
tatizo kama hilo hufikiri tofauti na kujiingiza katika mila potofu eti amerogwa,
ambapo amekemea hali hiyo na kuagiza jamii iachane na mambo hayo.
No comments:
Post a Comment