Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
IMEELEZWA kuwa asilimia 90 ya
familia wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, hutegemea kilimo na ufugaji katika
kuendesha shughuli za kimaendeleo katika maisha yao ya kila siku.
Aidha kati ya hizo asilimia 50
zinazalisha zao la kahawa wilayani humo, na ndio zao kuu ambalo hutegemewa kwa
kukuza uchumi wa wilaya hiyo.
Hayo yalisemwa na Kaimu mkurugenzi
mtendaji wa Halmashauri ya Mbinga, Oscar Yaspesa alipokuwa akisoma taarifa ya
maendeleo ya kilimo na mifugo kwa mgeni rasmi Diwani wa kata ya Mkako Ambrose Nchimbi
alipokuwa kwenye maonesho ya wakulima (Nane nane) yaliyofanyika katika kijiji
cha Lusonga wilayani humo.
Alisema mikakati ya kuendeleza sekta
hiyo muhimu ni pamoja na kuwaendeleza vijana katika kilimo na ufugaji ili
kuweza kuleta tija katika jamii.
Jumla ya Hekta 108,955 za mazao ya
chakula zilizalishwa katika msimu wa kilimo 2013/ 2014 na kwamba uzalishaji huo,
ulitokana na serikali kutoa vocha 55,350 za pembejeo za kilimo kwa wakulima.
Yapesa alisema pia huzingatia utoaji
wa elimu ya kilimo bora kwa wakulima kupitia shamba darasa, ambapo kufikia mwishoni
mwa mwezi Juni mwaka huu wilaya ina jumla ya vikundi 218 na maombi ya kuanzisha
vingine yanaendelea kupokelewa.
Alizitaja changamoto wanazokabiliana
nazo ni kutokuwa na soko la uhakika kwa mazao ya chakula yanayozalishwa
wilayani Mbinga, ikiwemo suala la uhaba wa wataalamu wa ugani na mifugo.
Pia bei kubwa za pembejeo za kilimo
nalo limekuwa tatizo sugu ambalo wakulima wengi wilayani humo, hushindwa kumudu
gharama ya kuzinunua na hivyo kushindwa kutosheleza mahitaji yao ya msingi.
Kwa upande wake Diwani Nchimbi
alisema umuhimu wa maonesho hayo ni kuwakutanisha wakulima, wadau wa kilimo,
mifugo, uvuvi na ushirika hivyo serikali itaendelea kushughulikia suala la
gharama kubwa ya pembejeo, ikiwemo kuwasiliana na taasisi mbalimbali nchini za
mikopo ili ziwakopeshe wakulima kwa gharama nafuu.
No comments:
Post a Comment