Na Kassian Nyandindi,
Ruvuma.
WADAU
wanaozalisha mazao ya chakula na biashara wilayani Mbinga na Nyasa mkoa wa
Ruvuma, wameitaka bodi ya leseni ya ghala Tanzania kuhakikisha kwamba
wanatekeleza mapema mfumo wa stakabadhi ghalani hususani kwa zao la kahawa, ili
kuweza kuzuia uharibifu na upotevu wa mazao wilayani humo.
Walisema
lengo la kufanya hivyo itasaidia walengwa wa mfumo huo ambao ni wakulima,
wafanyabiashara na vikundi husika kuweza kujijengea uwezo na hatimaye waweze
kuinua uchumi wao.
Ilielezwa
kuwa mfumo wa stakabadhi ghalani endapo utatekelezwa kwa haraka katika wilaya
hizo, utaleta fursa ya kufanyika kwa mnada wa zao la kahawa na kuuzwa katika
kipindi hiki cha msimu wa mavuno ya zao hilo.
Hayo
yalisemwa na Wadau hao walipokuwa kwenye mafunzo ya siku moja, yaliyofanyika
kwenye ukumbi wa Parokia Jimbo Katoliki la Mbinga uliopo mjini hapa ambayo
yalishirikisha wakulima, makampuni, maofisa ugani, vikundi mbalimbali na wadau
wa kahawa wa wilaya ya Mbinga na Nyasa.
“Lengo
letu hapa ni kumkwamua mkulima aweze kupiga hatua moja mbele katika sekta ya
kilimo, pia kutafuta soko na kuongeza thamani ya mazao yetu ili tuweze
kunufaika”, walisema.
Aidha
kwa upande wake Mratibu wa shirikisho la wakulima kutoka wilaya ya Nyasa
(MVIWATA) Ludwig Kumburu alieleza kuwa, katika kufanikisha jambo hilo aliitaka bodi ya
leseni ghalani hapa nchini kuwa karibu na maofisa ugani ili kuweza kuleta
ufanisi mzuri katika kazi.
Kumburu
alisema miundombinu ya kuwezesha mfumo wa stakabadhi ghalani kufanya kazi yake
umekuwa mgumu, hivyo ni vyema serikali ikaona umuhimu wa kuweka sawa suala hilo ikiwemo upatikanaji
haraka wa leseni ya umiliki wa ghala la kuhifadhia mazao husika.
Pamoja
na mambo mengine mwakilishi kutoka bodi ya leseni ya ghala Tanzania, Grace
Tarimo alisema elimu kwa wadau juu ya mfumo wenyewe unavyoendeshwa bado
haujawafikia wahusika ipasavyo hivyo bodi itafanya jitihada za kuweza kuweka
sawa jambo hili kwa kufikisha elimu kwa wadau husika.
No comments:
Post a Comment