Na Kassian Nyandindi,
Namtumbo.
SHIRIKA lisilo la kiserikali la kuendeleza watu wenye ulemavu na
watoto yatima Tanzania (SHIKUWATA) lenye makao yake makuu mkoani Ruvuma, limeendesha
mafunzo ya siku tano kwa watu wenye ulemavu na Watendaji wa kata ya Namabengo
Wilayani Namtumbo mkoani humo, kwa lengo la kuwafundisha juu ya kujua sera ya
maendeleo na huduma kwa watu wenye ulemavu.
Mafunzo hayo ambayo
yalifunguliwa na Diwani wa kata ya Namabengo wilayani humo Vitus Ngonyani,
ambayo yalifanyika katika ukumbi wa Namabengo Saccos uliopo mjini hapa na
kushirikisha wananchi mbalimbali wanaoishi kuzunguka eneo la kata hiyo.
Mratibu wa shirika hilo
Laura Martin akizungumza katika mafunzo hayo, alisema kuwa lengo la kutoa elimu
kwa walemavu hao ni kuwafanya wajue haki zao na wajibu wa kujihudumia pamoja na
kuangalia nafasi waliyonayo katika jamii na serikali kwa ujumla.
Laura alisema kuwa
washiriki hao katika kipindi chote cha siku tano watakachokuwa darasani wataweza
kujifunza mambo mbalimbali ikiwemo kujua hali ya watu wenye ulemavu, huduma za
watu wenye ulemavu, haki na ulinzi wa kisheria, dira na mwelekeo wa sera, matamko
ya sera kwa watu wenye ulemavu na mgawanyo wa majukumu katika ulinzi na usalama
kwa watu wenye ulemavu.
Naye Mkurugenzi wa
Shikuwata Magreth Mapunda, aliwataka washiriki hao kuwa watulivu na kufuatilia
kwa makini mafunzo hayo, ambayo mwisho wa siku yatawasaidia kujua haki zao na
kuwajengea uwezo wa kuweza kufuatilia masuala mbalimbali hususan serikalini na hata
katika jamii kwa ujumla.
Kwa upande wake mgeni
rasmi katika ufunguzi wa mafunzo hayo Diwani wa kata ya Namabengo Vitus Ngonyani,
aliwataka wananchi kuwaona watu wenye ulemavu kama sehemu ya jamii ya
Watanzania na wana haki sawa na watu wengine.
Ngonyani aliongeza kwa
kuitaka jamii kuacha tabia ya kuwabagua na kuwanyanyapaa watu wenye ulemavu,
badala yake amewahimiza kuwa mstari wa mbele katika kuwasaidia wanapopambana na
changamoto mbalimbali ikiwemo kuwasaidia fedha kwa ajili ya matibabu, usafiri,
chakula na elimu.
Kwa upande wao walemavu
hao kwa nyakati tofauti walisema kuwa wanakabiliwa na matatizo hayo ikiwemo
kutokuwepo kwa usawa katika mgawanyo wa rasilimali za taifa, ugumu wa kupata
nafasi za ajira pindi zinapotokea, pamoja na kupata usumbufu mkubwa katika
upande wa kupata matibabu pale wanapokwenda kutibiwa kwenye vituo vya afya au
hospitali za serikali.
No comments:
Post a Comment