Na Mwandishi wetu,
Tunduru.
WAZAZI na Walezi wilayani Tunduru mkoa wa
Ruvuma, wameaswa kushirikiana na serikali kusimamia na kufuatilia
kwa karibu mienendo na maendeleo ya watoto wao hasa wa kike, ikiwa ni juhudi ya
kuhakikisha kuwa watoto hao wanafanya vizuri katika masomo
yao na kujiletea maendeleo yao.
Ofisa mtendaji wa kata
ya Mhuwesi Shijabu Ngoronje alisema hayo wakati alipokuwa
akizungumza kwenye mkutano wa Wadau wa elimu uliofanyika katika Kijiji cha
Mhuwesi, ukiwa ni mwendelezo wa juhudi za mradi wa usimamizi na utetezi
wa haki ya mtoto wa kike kupata elimu .
Akifafanua taarifa hiyo Ngoronje alisema,
ili kufanikisha adhima hiyo serikali imejipanga kutoa elimu kwa kuwaomba wazazi
na walezi kujitoa kuchangia chakula cha mchana kama kivutio kwa watoto
wao na kuwafanya wapende masomo.
Kuhusu mila na desturi za makabila ya
Wayao wilayani Tunduru, alisema kuwa tayari serikali imeunda kikosi kazi cha
kuonana na viongozi wa mila, makungwi na manyakanga na kuwaomba wasaidie
kuiwaelimisha juu ya utoaji wa elimu kwa watoto wa kike, na kuwafanya wapende
masomo tofauti na sasa ambapo kundi hilo limekuwa likifundishwa kukabiliana na
maisha ya ndoa hali inayosababisha kuwepo kwa matukio mengi ya ndoa za utotoni
wakiwa shuleni.
Kuhusu wazazi wenye tabia za kutunza siri
za watoto wao wakike baada ya kupewa mimba na wanaume kwa kisingizio cha kutaka
kuwaozesha mapema alisema , serikali imejipanga kupambana nao kwa kuanza
kuwachukulia hatua wazazi na watoto husika pamoja na manyakanga ambao wamekuwa
wakitoa mafunzo mabaya wakati wa jando na unyago.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya
washiriki wa mafunzo hayo Hakimu Kilowa na Hussein Makoroboyi
katika maoni yao juu ya kinacho sababisha elimu kushuka wilayani humo,
walidai kuwa Kipato duni cha akina mama ndio chanzo kikuu, ambapo mara nyingi
ndio wamekuwa wakiachiwa jukumu la kutunza watoto wa kike .
Aidha wadau hao pia
wakatumia nafasi hiyo kuwashukuru kuwapongeza wafadhili wa mradi huoShirika
la The Foundation for Civil Society (FCS) la Jijini Dar Es Salaam, kwamba mradi huo utaweza kuongeza msukumo
kwa wazazi kuwahimiza watoto wao kwenda shule, pia kuwa apunguzia majukumu
watoto wa kike na kuwaoza mapema kabla ya umri wao.
Shekhe mkuu wa Tunduru
Alhaji Waziri Chilakwechi alipongeza kuwepo kwa mradi huo, ambao alisema
kuwa ni ukombozi kwa mtoto wa kike na utaweza kuongeza msukumo kwa wazazi
kuwahimiza watoto wao kwenda shule, pia kuwapunguzia majukumu watoto wa kike na
kuwaoza mapema kabla ya umri wao.
Awali akitoa taarifa ya mradi huo
Meneja wa mradi wa shirika kiserikali la TUFAE Education Aids Trust,
linalo simamia uhamasishaji huo John Nginga alisema kuwa mradi
huo ulibuniwa kufuatia majibu mabaya ya utafiti uliofanywa na shirika hilo
mwaka 2007 hadi 2010 na kubaini uwepo wa maendeleo mabaya ya elimu kwa mtoto wa
kike wilayani humo, na kuchukua uamuzi wa kuhakikisha kuwa mtoto wa kike
anapata elimu kuanzia darasa la awali, elimu ya msingi, sekondari hadi
Chuo Kikuu.
Nginga aliendelea kubainisha kuwa katika
utafiti huo uliofanyika katika tarafa za Muhuwesi, Namasakata, Ligoma, Nandembo,
Mlingoti Mashariki na Mlingoti Magharibi wilayanbi Tunduru zilibainisha
kuwapo kwa kundi kubwa la watoto wa kike waliopata mimba pamoja na kikwazo cha
uelewa mdogo wa jamii juu ya sera ya elimu, haki ya mtoto wa kike kupata elimu
na mila zilizopitwa na wakati.
Takwimu hizo zilifafanua kuwa katika
kipindi cha mwaka 2007 hadi 2010 jumla ya waliotarajiwa kuandikishwa shule ni
watoto wa kike 17,386, walioandikishwa ni 14,692 ambao ni sawa na asilimia
85.49% na waliosajiliwa ni 13,411, na waliofanya mitihani wa kumaliza
darasa la saba walikuwa 13,097 ambao ni sawa na asilimia 97.65%, huku kukiwa na
anguko la watoto 314 ambao waliacha shule kwa sababu mbalimbali ikiwemo kupata
mimba wakiwa shuleni pamoja na utoro.
No comments:
Post a Comment