Baadhi ya Wajumbe ambao ni Watu wenye ulemavu, wakimsikiliza kwa makini mgeni rasmi(hayupo pichani) wakati alipokuwa akihutubia katika mkutano wao. |
Mwenyekiti wa CHAWATA Songea mjini, ambaye amesimama Kassim Mgwali akisisitiza jambo kwa kuitaka serikali, izingatie uwepo wa mahitaji muhimu kwa watu wenye ulemavu. (Picha zote na Kassian Nyandindi) |
Na Kassian Nyandindi,
Songea.
IMEBAINISHWA kuwa changamoto kubwa inayoathiri maendeleo ya watu
wenye Ulemavu mkoani Ruvuma, ni unyanyapaa uliokithiri katika nyanja mbalimbali,
ikiwemo mazingira magumu ya kupata elimu na kuwezeshwa kiuchumi kuweza kupata nafasi ya
kuingia katika vyombo vya maamuzi.
Aidha uongozi wa halmashauri za mkoa huo umetupiwa lawama
kwamba umekuwa ukiwatenga kundi la watu hao, pale wanapohitaji msaada au
ufafanuzi wa mambo mbalimbali.
Kufuatia hali hiyo, serikali imeombwa kuingilia kati na
kuhakikisha tatizo hilo linafanyiwa kazi ikiwemo ushirikishwaji kwa watu wenye
ulemavu katika kupanga bajeti ya maendeleo kwa ngazi mbalimbali, uwe unatekelezwa
ipasavyo.
Hayo yalibainishwa na Wajumbe wa mkutano Mkuu wa uchaguzi wa
viongozi wa ngazi ya mkoa wa Ruvuma, uliofanyika leo kwenye ukumbi wa Halmashauri
ya wilaya ya Songea uliopo mjini hapa na kuhudhuriwa na mgeni rasmi afisa
maendeleo ya jamii wa mkoa huo, Anton Nginga.
Mjumbe wa kutoka wilaya ya Namtumbo ambaye ni Mwenyekiti wa
Chama Cha Walemavu(CHAWATA) wilayani humo, Ibadi Naimu alisema ni jambo la
kusikitisha kwa viongozi wa mkoa huo kuwatenga na kutoshirikisha ipasavyo watu
wenye ulemavu hivyo ni vyema kuanzia sasa pawepo na mabadiliko ili kundi hilo liweze
kusonga mbele kimaendeleo.
“Serikali ya mkoa wa Ruvuma sisi walemavu mnatutenga, kitendo
hiki kinasikitisha sana”, alisema Naimu.
Kadhalika waliuomba uongozi wa mkoa huo kupitia halmashauri
zake, kutenga maeneo maalum kwa ajili ya watu wenye ulemavu kufanyia shughuli
mbalimbali, ikiwemo zile za ujasiriamali.
Naye Mgeni rasmi Afisa maendeleo ya jamii wa mkoa wa Ruvuma
Bw. Nginga kwa upande wake alisema, atafikisha kilio hicho cha watu wenye
ulemavu sehemu husika ili kiweze kufanyiwa kazi.
“Ndugu zangu sisi wenyewe kwanza ni lazima tujikomboe
kifikra, tusijiweke nyuma katika kupigani haki zetu”, alisisitiza Nginga.
Pamoja na mambo mengine aliongeza kuwa Viongozi wa CHAWATA kwa
kushirikiana na Wakurugenzi wa halmashauri za mkoa huo, watumie fursa za mifuko
ya Wanawake na Vijana kujiunga katika vikundi na kuweza kukopa fedha ambazo
zitawasaidia kuendesha miradi ambayo wameibuni kutoka katika vikundi husika,
ili iweze kuwa kwamua kiuchumi.
Wajumbe hao wa CHAWATA mkoa wa Ruvuma waliweza kuchagua
viongozi wao wa kuweza kuwaongoza katika kipindi cha miaka mitano ambao ni
Mwenyekiti Samwel Mapunda aliyepata kura 10 na kumbwaga chini mpinzani wake
Aidan Mhone aliyepata kura 7.
Makamu Mwenyekiti aliyeshinda ni Elepord Haulle kura
aliyepata kura 11 na mpinzani wake alipata kura 6, Katibu mkuu Polycard Tossi
kura 9 na kumbwaga chini Ally Kiponda aliyepata kura 8 na kwa nafasi ya Katibu msaidizi ilishindaniwa
na Mashaka Mboya kura 9 na kumbwaga chini Rajabu Mwera aliyepata kura 8.
Nafasi ya Mweka hazina ilinyakuliwa na Christina Mwinuka
aliyepata kura 11 na kumbwaga chini mpinzani wake Erick Nyoni aliyepata kura 6
na kwamba nafasi ya Wajumbe wa kamati tendaji walioshinda ni sita kati ya wagombea
11 waliokuwa wakiwania nafasi hiyo.
No comments:
Post a Comment