Monday, November 18, 2013

KATIBU MKUU WA CCM TAIFA AKUMBANA NA KERO YA KOROSHO TUNDURU, WATENDAJI WIZARA YA KILIMO WATILIWA SHAKA

Na Steven Augustino,
Tunduru.

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Taifa Abrahaman Kinana ambaye anaendelea na ziara yake wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, amekutana na kero inayoendelea kulitesa Soko la korosho huku wananchi wa wilaya hiyo wakilalamikia kwamba tatizo hilo kutokana na kudumu kwa muda mrefu, linawafanya wakose imani na Wizara ya kilimo chakula na ushirika ambayo ilipaswa kusimamia.


Kufuatia hali hiyo Kinana naye ilimlazimu kutilia shaka utendaji wa Wizara hiyo na kuahidi kuwa litafanyiwa utekelezaji wa haraka ili kuondoa kero hiyo iliyopo sasa. 


Kilio hicho cha Wakulima wa korosho wilayani Tunduru kilijitokeza katika vijiji vya Lukumbo, Munjaku, Mchoteka, Nalasi na Mtina vilivyopo katika Jimbo la Tunduru Kusini wilayani humo.  



Kufuatia hali hiyo Kinana aliwahakikishia  Wakulima wa zao hilo katika mikoa na wilaya zinazolima zao hilo hapa nchini kwamba, hatua madhubuti zitachukuliwa katika kunusuru halo lisiweze kuendelea, huku akiongeza kuwa anahakika linatokana tu na uzembe wa viongozi wachache waliopo madarakani kutotekeleza majukumu yao ipasavyo na kutomthamini mchango wa mkulima katika taifa hili.


Alisema tatizo hilo CCM imelibaini kwa muda mrefu na inalifanyia kazi ili kuweza kuepukana na wanunuzi wa zao hilo ambao wanaonekana kufanya  ubabaishaji, ulaghai, wizi na udanganyifu wakati wa msimu wa ununuzi wa zao hilo ambao unalenga kudumaza maendeleo ya zao hilo na mkulima kwa ujumla.


Akihutubia kwa utaratibu wa kuuliza maswali juu ya kero hiyo Katibu mkuu wa chama hicho Bw. Kinana  alisema endapo serikali itaendelea kuwakumbatia viongozi wazembe, taifa hili litakuwa katika hali mbaya huku akieleza kuwa kamwe CCM haitakubali kuona mambo kama haya yanaendelea kufumbiwa macho.



“zao la Korosho hivi sasa limeingiliwa na usanii mwingi unaoambatana na vitendo vya wizi, unyang’anyi na udanganyifu ambao umekuwa ukifanywa na wajanja wachache, sasa ninasema hatua za haraka zitachukuliwa katika kudhibiti hili", alisisitiza. 

No comments: