Sunday, November 24, 2013

WAJASIRIAMALI WAMPA PONGEZI DIWANI WAO



Na Steven Augustino,
Tunduru.

KIKUNDI cha akina mama wajasiriamali wa tawi la Majengo B wilayani  Tunduru mkoa wa Ruvuma, kimempongeza Diwani wa kata ya Majengo  Athuman Nkinde kwa moyo wake wa kujitoa na kufanikisha utekelezaji wa miradi mbalimbali wilayani humo, ambayo aliahidi wakati wa kuwania nafasi hiyo mwaka
2010.

Mwenyekiti wa tawi la Majengo B la Chama cha Mapinduzi (CCM) Fatuma Mtesa alisema hayo wakati akisoma taarifa ya utekelezaji wa Mafunzo ya uzalishaji mali, kwa wanakikundi hao katika hafla fupi iliyofanyika viwanja vya ofisi za CCM katani humo.

Mtesa alisema kuwa katika mafunzo hayo ya siku 10 jumla ya akina mama wajasiriamali 46 walishiriki, ambapo yalitolewa chini ya ufadhili wa diwani Nkinde.


Alifafanua kuwa katika kipindi hicho akina mama hao walijifunza jinsi ya kutengeneza batiki, mafuta na sabuni.
 
Pamoja na Diwani huyo kujitolea kuwahudumia wananchi wake pia kikundi hicho alianza kukifadhili kwa kuwawezesha kulima shamba la mpunga na kuwapa pembejeo za kilimo, kuanzia msimu wa kilmo wa mwaka 2012/2013.

Kwa upande wake diwani Nkinde pia aliwataka wanavikundi wa mataawi ya Muungano, Majengo A na Kalanje wilayani Tunduru, kuwa na moyo wa subira ambapo nao aliwaahidi  kuwapelekea mafunzo ya aina hiyo ili wawe wabunifu wa miradi mbalimbali katika maeneo yao na waweze kuondokana na umasikini katika   familia zao.

No comments: