Mazingira yanavyoharibiwa kama hivi, ni hatari kwa maisha ya binadamu na viumbe hai. |
Na Kassian Nyandindi,
Songea.
WANANCHI waishio mkoani Ruvuma, wameshauriwa kuwa na tabia ya kutunza mazingira pamoja na vyanzo vya maji na
kuvifanya kuwa endelevu, kwa faida ya vizazi vijavyo na hata kwa
matumizi yao wenyewe ili waweze kuwa na maisha endelevu.
Hivi sasa kumekuwa na
kasi kubwa ya uharibifu wa vyanzo hivyo kunakosababishwa na shughuli za
kibinadamu kama vile kilimo na ufugaji hali ambayo inatishia kutoweka kwa uoto
wa asili.
Wito huo ulitolewa na
mshindi wa tuzo ya mazingira ambaye pia ni mwanaharakati wa msuala
ya mazingira na uhifadhi wa vyanzo vya maji mkoani Ruvuma, Menas Andoya
alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mjini Songea, kuhusiana na
kasi kubwa ya uchomaji moto misitu na uchafuzi wa vyanzo vya
maji ambao umeshamiri mkoani humo.
Alisema viongozi kuanzia
ngazi ya vitongoji, vijiji na hata kata wanapaswa kusimamia
kikamilifu suala la utunzaji wa mazingira pamoja na vyanzo vya maji kutokana na
wao ndiyo wanaoishi na wananchi.
“Kila siku baadhi ya
wananchi kazi yao ni kukata miti na kulima katika vyanzo vya maji ambavyo ni
tegemeo kubwa kwa maisha ya binadamu na wanyama hai, inatakiwa sasa jamii
ibadilike ili tuweze kuondokana na ukame unaoweza kujitokeza hapo baadaye”,
alisema Andoya.
Vilevile amesikitishwa
na hali ya mazingira ilivyo katika wilaya mbalimbali hapa mkoani Ruvuma, ambapo
wananchi wanachoma moto misitu na kukata miti kwa wingi ambayo ni tegemeo kubwa
kwa mvua ili iweze kunyesha huku wakishindwa kupanda mingine na kusababisha
maeneo mengi kuwa jangwa.
Alifafanua kuwa kutokana
na utafiti alioufanya miaka kadhaa iliyopita, amebaini kuwepo kwa baadhi
ya viongozi wa ngazi za chini yaani vijiji na kata kuwa wamekuwa wakishiriki
katika uharibifu huo, na kuwahamasisha wananchi kulima kwenye vyanzo vya maji
kwa maslahi yao binafsi ya kisiasa na kutaka umaarufu usiokuwa na faida kwa
watu wengine.
Andoya alisema,tabia
hiyo imechangia sana kuwepo kwa uhaba mkubwa wa maji katika maeneo mbalimbali,
na kama hakutakuwa na hatua madhubuti zitakazochukuliwa katika
kudhibiti hilo, hali inaweza kuwa mbaya zaidi.
Pamoja na mambo mengine
ameishauri serikali kupitia mamlaka husika za maji na mazingira
mkoani Ruvuma, kuendesha semina za utunzaji wa mazingira na vyanzo vya maji
hususani maeneo ya vijijini ambako ndiko kwenye idadi kubwa ya waharibifu wa vyanzo vya maji
na mazingira.
No comments:
Post a Comment