Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Shukuru Kawambwa. |
Na Kassian
Nyandindi,
Ruvuma.
HATIMAYE Baraza la Madiwani katika Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, limefanya maamuzi mazito ya kumkataa Afisa Elimu Taaluma wa wilaya hiyo Rashid Pilly, na kumwagiza Mkurugenzi na Mwenyekiti wake wa halmashauri hiyo kumwondoa haraka afisa huyo na kumrejesha kwa Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya ufundi.
Pilly analalamikiwa kwa muda mrefu
kutokana na kile kinachoelezwa kuwa ni kikwazo katika utendaji kazi wa idara
hiyo, amekuwa akitumia muda mwingi badala ya kufanya kazi husika, yeye amekuwa
akiandika barua zenye kuzua migogoro, kuchafuana na kugombanisha wafanyakazi
wenzake na afisa elimu wa wilaya hiyo Mathias Mkali.
Hatua ya Madiwani hao kumkataa Afisa
elimu taaluma wa wilaya hiyo, imejitokeza hivi karibuni katika kikao cha Baraza
hilo kilichoketi kwenye ukumbi wa Jumba la Maendeleo, uliopo mjini hapa.
Makamu Mwenyekiti wa Baraza la
Madiwani wilayani Mbinga ambaye alikuwa akiendesha kikao hicho, Winfrid Kapinga
alisema wamekasirishwa na tuhuma hizo na kubaini kwa muda mrefu kuwa vitendo
hivyo vinavyofanywa na Pilly, vinaweza kudumaza mikakati iliyowekwa ya
kimaendeleo katika kukuza elimu wilayani humo.
Kapinga alifafanua kuwa Afisa elimu
msingi wa wilaya hiyo Bw. Mkali alipohamia wilayani Mbinga mwaka 2011 aliweza
kuinua kiwango cha taaluma kutoka asilimia 40 hadi kufikia asilimia 53.6 na
kuifanya halmashauri hiyo kushika nafasi ya pili mkoani Ruvuma, kati ya wilaya
tano zilizopo mkoani humo.
“Tumeamua kumkataa huyu mtu kutokana
na matendo yake, ni vyema arejeshwe kwenye mamlaka yake ya uteuzi ili kuondoa
migogoro hii ambayo imekuwa kero kubwa katika idara hii ya elimu”, alisema
Kapinga.
Mwenyekiti huyo aliongeza kuwa Mkali
alipohamia wilayani Mbinga, aliweza kukabiliana na tatizo la watoto 1,744
wasiojua kusoma, kuandika na kuhesabu (KKK) kwa kuweka mikakati madhubuti
ambayo ilishirikisha walimu wote mashuleni na kuifanya wilaya hiyo iweze
kusonga mbele.
Pamoja na mambo mengine, Diwani wa
kata ya Litembo Altho Hyera alipozungumza na Waandishi wa habari nje ya ukumbi
wa mikutano, alisema hatua iliyochukuliwa na baraza hilo inapaswa kuungwa mkono
huku akieleza kuwa Pilly amekuwa akiendeleza migogoro ya kuandika barua hizo,
kwa kushirikiana na Katibu wa Chama Cha Walimu Tanzania (CWT) tawi la Mbinga
Samwel Mhaiki na kuufanya uongozi wa wilaya hiyo kushindwa kufanya kazi zake za
kimaendeleo, kutokana na muda mwingi kuutumia kujibu tuhuma wanazoziandika
katika barua hizo na kuzipeleka ngazi ya juu.
“Huyu Pilly muda mwingi yeye badala
ya kufanya kazi anafikiria kuandika mabarua ya kuchafuana yasiyo na faida
kwetu, kamati husika iliundwa kufuatilia jambo hili na imebaini kuwa hakuna
ukweli wa mambo anayo andika na sisi tumeona hatufai………..aondoke”, alisema
Hyera.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya elimu,
afya na maji wilayani Mbinga ambaye ni Diwani wa kata ya Litumbandyosi, James
Yaparama alieleza kuwa wamechoshwa na mambo yaliyofanywa na afisa elimu taaluma wa wilaya hiyo hivyo
hawaoni sababu ya kuendelea kukaa na mtu ambaye muda mwingi amekuwa akileta
matatizo katika wilaya yao ambayo yakiendelea kufumbiwa macho huenda maendeleo
katika sekta ya elimu yakarudi nyuma.
Hata hivyo alipoulizwa Pilly
alieleza kuwa yeye tuhuma hizo anazisikia tu watu wakizungumza mitaani na bado
hajapata barua rasmi ya kumuhamisha katika kituo chake cha kazi kutoka kwa
mwajiri wake, huku akiongeza uamuzi uliochukuliwa na baraza hilo hautambui na
ataendelea na kazi kama kawaida ambapo vilevile alipotafutwa kwa njia ya simu
Katibu wa CWT tawi la Mbinga, Samwel Mhaiki ili aweze kujibia suala la
kuhusishwa na tuhuma hizo, hakuweza kupatikana na simu yake ilikuwa imefungwa
kwa muda mrefu.
No comments:
Post a Comment