WAZIRI wa Maendeleo ya
Mifugo na Uvuvi Dokta Titus Kamani, amesema ili kwenda na kasi ya maboresho ya
wizara hiyo, inahitajika dhana ya uwajibikaji na uwazi sambamba na kujitolea
kwa nguvu zote katika kufanya kazi.
Kamani, aliyasema hayo
juzi katika mkutano wa kwanza uliowakutanisha wafanyakazi wote wa wizara hiyo,
wakiwemo wastaafu wa mwaka jana katika ofisi ya wizara hiyo ilizopo Temeke
jijini Dar es Salaam.
Alisema kama kuna mtu ambaye ni
kikwazo katika kukwamisha shughuli za wizara, ni bora akawapisha mapema na
kwamba kila mtumishi kwa nafasi yake, anatakiwa kuifanya kazi kwa uwazi na
akaitaka wizara kufanya kazi na vyombo vya habari kwani ndio njia pekee ya
kuwafanya watanzania wajue wizara inafanya nini.
“Wewe upo ofisini, halafu
unaogopa ogopa vyombo vya habari, kwani unatatizo gani kuweni wazi mambo yenu
yawe hadharani watanzania wa Mbeya wayajue, Rufiji mpaka Pemba, hakuna kuficha
ficha jambo katika wizara yangu.” alisistiza Dokta Kamani.
Alisema wizara ya maendeleo ya
mifugo na uvuvi ndio moyo wa taifa kwani huwajumuisha watanzania wengi wenye
maisha ya kawaida, lakini amesikitishwa kwa jinsi ambavyo wizara hiyo imekuwa
ikichukuliwa na baadhi ya watu kama ni wizara yenye migogoro na kuleta hasara
maeneo mengine.
“N'gombe hawa wamekua wakiingia
kwenye hifadhi, wanapigwa risasi, wanaaribu mashamba ya watu na kuleta njaa kwa
wananchi, ng'ombe hawa wamekuwa wakisema wanaleta uharibifu wa mazingira kwa
wananchi kwa sababu ya kuhamahama, kama ng’ombe hawa ungepatikana utaratibu
mzuri wa kuwatunza na kuwahifadhi basi, taifa hili lingeingiza kipato kikubwa
ikiwemo kuuza nyama hadi nje ya nchi, maziwa na kuboresha afya za watanzania”
alisema Dokta Kamani.
Dokta Kamani, amesema anafahamu
wizara yake ina changamoto nyingi katika kutekeleza majukumu yake ikiwemo
bajeti kuwa ndogo, lakini kwa kutumia taaluma yake pamoja na ushirikiano wa
wafanyakazi wote wa wizara hiyo, anaamini itakuwa ni wizara yenye neema kwa
watanzania, yenye kueneza ajira na kipato kwa sababu hakuna jambo
lisilowezekana kama kila mmoja atafanya kazi kwa dhamira moja.
Akizungumzia juu ya ranchi za
taifa, waziri Kamani amesema ana nia ya dhati ya kuona ranchi za taifa
zinafufuka na kutengeneza uchumi imara wa taifa, kuzalisha ngombe wenye ubora
ambao watatoa mazao ya mifugo yatakayoliingizia taifa hili kipato kikubwa.
Akizungumzia sekta ya uvuvi
Waziri Kamani alisema sekta hiyo ni tabu tupu alisema leo tunaambiwa kuna uvuvi
haramu, nyavu zisizokidhi viwango na huku wavuvi wakiendelea kuwa masikini,
katika nchi yenye bahari, maziwa na mito mikubwa kila kona, ameuliza ni kweli
wanahitaji bajeti kubwa ya kushughulika na mambo hayo?.
“Tunahitaji utashi wa kuwasadia
wavuvi wetu, kwa kutoa elimu na kufanya mazungumzo nao ya mara kwa mara,
kuwatembelea maeneo yao ya kazi na kubaini matatizo yao kisha kuyafanyia kazi”,
alibainisha.
Kuhusu zao la kuku Waziri
Kamani alisema hivi sasa kuna tatizo la mayai feki na chanjo feki, alihoji ni
kweli kwamba wafanyakazi wa wizara hiyo haiwajui wahusika au kuna baadhi ya
watumishi ndio miradi yao? ambapo aliagiza wizara kubaini wanaofanya biashara
hiyo feki ambayo inaleta madhara hasa wakazi wa mjini ambao ni watumiaji wakubwa
wa bidhaa hizo.
No comments:
Post a Comment