Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
BAADHI ya Wanaume wa kijiji cha
Mbangamao kati, kata ya Mbangamao wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma wamezikimbia
familia zao wakihofia kukamatwa na polisi baada ya kuvamia nyumba ya Mratibu
elimu wa kata hiyo Florence Kowelo, na kumjeruhi kwa kumpiga nondo kichwani.
Watu hao wanadaiwa kufanya kitendo
hicho na kutishia usalama wa Watumishi wengine wa serikali, katika kata hiyo
baada ya kuwatuhumu wamekuwa na tabia ya kufanya mapenzi na wake zao.
Tukio hilo lilitokea usiku wa
Desemba 27 mwaka huu na kwamba vibaka hao ambao wanatamba kijijini hapo kwa
jina la M 23, kuwa wameapa kupambana na Watumishi wote waliopo katika kata ya
Mbangamao.
Akizungumza na mwandishi wa habari
hizi Ofisa mtendaji wa kata hiyo Elnea Mwanyekule alisema Wanaume hao ambao
majina yao hakutaka kuyataja kwa sababu za kiusalama, wamezikimbia familia zao
na kwenda kusikojulikana baada ya kutokea vurugu hizo.
“Hivi sasa amani na utulivu katika
eneo hili imekuwa ni tatizo, watu Wafanyakazi tunaishi kwa wasiwasi kutokana na
kundi hili ambalo limekuwa likitamba muda mwingi kuwa litaendelea kupambana na
watumishi waliopo hapa”, alisema.
Kuhusu madai ya kwamba Watumishi wa
kiume waliopo katika kata hiyo wanatabia ya kufanya mapenzi na wake za watu,
Mwanyekule alikanusha na kusema kuwa kauli hizo si za kweli bali kundi hilo
litakuwa na sababu zingine ambazo yeye hazifahamu.
Diwani wa kata ya Mbangamao
Christantus Mbunda, naye alipozungumza na mwandishi wa habari hizi
alithibitisha kuwepo kwa vurugu hizo na kusema kuwa tayari hatua za kulisaka
kundi hilo zinafanyika, kutokana na vibaka hao kuendelea kuleta vitisho vya
kutaka kumuua mwalimu mkuu wa shule ya msingi Mbangamao Mathayo Kivinga.
Mbunda alisema hatua za awali
zimechukuliwa kwa kumuhamisha Mratibu elimu wa kata hiyo ambaye amejeruhiwa na
mwalimu huyo wa shule ya msingi, ili kuweza kunusuru maisha yao wakati taratibu
zingine za kisheria zinaendelea kuchukua mkondo wake.
Kamanda wa polisi wa mkoa wa Ruvuma
Deusdedith Nsimeki amesema jitihada za kuwasaka vibaka hao zinaendelea
kufanyika, na kuongeza kuwa taratibu husika zitakapokamilika watafikishwa
Mahakamani.
No comments:
Post a Comment