Na
Kassian Nyandindi,
Songea.
UJENZI wa barabara kiwango
cha lami kuanzia eneo la Likuyufusi pacha ya Peramiho wilaya ya Songea hadi
Mbinga, umeanza kuzua malalamiko kutokana na barabara hiyo kuanza kuwekwa
viraka kabla ya kukabidhiwa rasmi mikononi mwa serikali.
Barabara
hiyo ambayo ni ya kilometa 78 inagharimu kiasi cha shilingi bilioni 79.8 na kutekelezwa
chini ya mradi mkuu wa changamoto za milenia Tanzania (MCAT).
Fedha
za ujenzi wa barabara hiyo ni miongoni mwa dola 698 za Kimarekani zilizotolewa
nyakati za mwisho katika utawala wa Rais mstaafu George Bush, ikiwa ni sehemu
ya msaada kwa ajili ya kujenga miradi mbalimbali ya kimaendeleo hapa nchini.
Malalamiko hayo yalitolewa kwa nyakati
tofauti wakati mwandishi wa habari hizi alipokuwa akizungumza na wananchi wa
Songea na Mbinga, ambapo walisema kuwa ni jambo la kushangaza kuona ujenzi wa
barabara hiyo kabla haijakabidhiwa rasmi imeanza kuwekwa viraka baadhi ya
maeneo.
“Kwa
kweli hatukutarajia kama leo hii barabara inajengwa kwa kiwango cha lami halafu
kabla ya kukabidhiwa rasmi mikononi mwa serikali inabomoka na kuwekwa viraka,
maana viongozi walituhakikishia barabara yetu itajengwa vizuri na kwa kiwango
bora”, walisema.
Kampuni ya Sinohydro Corporation Limited
kutoka nchi ya China , ndiyo imekabidhiwa kazi ya ujenzi wa kiwango cha lami na kwamba ujenzi wake hadi kukamilika umechukua
zaidi ya miezi 27.
Huu
ni mradi mkubwa wa pili hapa mkoani Ruvuma, wa ujenzi wa barabara kwa kiwango
cha lami ambao umetanguliwa na mradi mwingine wa ujenzi wa barabara ya lami kutoka
Songea hadi Namtumbo ikiwa ni utekelezaji wa maendeleo ukanda wa Mtwara.
Utekelezaji huo ambao umepewa jina maarufu
“Mtwara Corridor” umelenga kuunganisha barabara kwa kiwango cha lami kutoka
bandari ya Mtwara, bahari ya Hindi hadi bandari ya Mbamba bay ziwa Nyasa wilayani
Mbinga.
Hata
hivyo Mwandishi wa habari hizi alipomfuata Meneja wa Wakala wa barabara
Tanzania (TANROADS) mkoani Ruvuma Abraham Kissimbo ofisini kwake, ili aweze
kutoa ufafanuzi juu ya malalamiko hayo alimtuma muhudumu wake wa ofisi na
kumweleza kuwa hana nafasi ya kuweza kuzungumza na mwandishi wa habari hizi.
No comments:
Post a Comment