Tuesday, December 17, 2013

ABIRIA TUNDURU WALALAMIKIA KUNYANYASWA, SUMTRA YAOMBWA KUINGILIA KATI



Na Steven Augustino,
Tunduru.

WADAU na Abiria ambao hufanya safari zao kutoka wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, kwenda jijini Dar es Salaam wamelalamikia kutozwa nauli za mabegi jambo ambalo linasababisha usumbufu mkubwa kwao.

Sambamba na tukio hilo pia wasafiri hao walidai kuwa wamekuwa wakitukanwa na kutolewa lugha chafu na wafanyakazi wa mabasi ambayo hufanya safari katika ukanda huo wa kusini.

Kilio cha wasafiri hao kiliwasilishwa na Leonsi Kimario wakati akizungumza na maafisa wa Mamlaka ya udhibiti wa usafiri wa nchi kavu na majini (SUMATRA) katika kikao kilichofanyika ukumbi wa New Generation bar uliopo mjini hapa.
   
Kimario ambaye alionekana kuungwa mkono na wajumbe wengi waliohudhuria mkutano huo, alisema abiria hao wamekuwa wakitozwa fedha  kati ya shilingi 10,000 na 5,000 kama malipo ya nauli ya mabegi yao hali ambayo imekuwa ikiwakwaza abiria wengi ambao hufanya safari zao kutoka katika maeneo hayo.

 
Wakijibu kero hizo kwa nyakati tofauti Afisa mfawidhi wa SUMATRA  mkoa wa Ruvuma   Denice Daudi na mkuu wa usimamizi wa kitengo cha usalama barabarani wilayani Tunduru Asp Lilanga Chodas, pamoja na kutoa maelekezo mbalimbali ya kisheria wanayopaswa kuyafuata wasafirishaji wa abiria kote nchini, aliwataka Wananchi kujenga tabia ya kujisomea vipeperushi kwa ajili ya kutambua haki zao za msingi pamoja na kutoa ushirikiano kwa  mamlaka husika, ili kuwakamata wamiliki wa magari hayo ya abiria ambao wanakikuka sheria.

Daudi aliendelea kueleza kuwa hivi sasa serikali kupitia Wizara ya uchukuzi, imejipanga kuwashughulikia wamiliki na watumishi wa vyombo hivyo vya usafiri wanaokiuka kanuni ya 18 ya sheria namba 128 ya mwaka 2007 inayowakataza kuwafanyia ukatili na kuwanyanyasa abiria wao, na kusisitiza kuwa abiria atakayefanyiwa vitendo hivyo atoe taarifa kituo chochote cha polisi kilichokuwa jirani.

Vilevile naye Denice alitolea mfano kuwa abiria anayetoka Dar es salaam kwenda wilayani Tunduru, ioneshe kuwa abiria husika amelipa nauli halali iliyoidhinishwa na mamlaka hiyo kuwa ni shilingi 32,000 na kwamba tiketi ambazo zitabainika kuwa abiria huyo ametozwa zaidi ya kiwango hicho ziwasilishwe SUMATRA au atoe ushirikiano kwa mamlaka kwa ufuatiliaji wa haki hizo na ikibainika basi husika ambalo limefanya hivyo, litatozwa faini ya shilingi 250,000.  

Alisema hadi sasa mamlaka hiyo imefanikiwa kuwakamata baadhi ya wasafirishaji wanaotoza nauli kubwa katika njia ya Tunduru kwenda Songea ambapo abiria walikuwa wakitozwa nauli tofauti hivyo wameweza kuwachukulia hatua za kisheria ili iwe fundisho kwa wengine wenye tabia kama hiyo.

Hata hivyo akifunga mkutano huo Mwenyekiti wa chemba ya wafanyabishara (TCCIA) wilayani Tunduru   Mussa Ndeka aliwataka wasafirishaji kufuata taratibu na sheria zilizowekwa, ili kuepusha usumbufu ambao unaweza kujitokeza baadaye. 

No comments: