Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
IMEELEZWA kuwa kukosekana kwa shule maalum kwa watu wenye
ulemavu wa aina mbalimbali wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, kunasababisha watu
hao kukosa haki zao za msingi za kupata elimu, ambayo ingelifanya kundi hilo,
kuweza kuondokana na maadui wawili ujinga na umasikini.
Kutokana na ukosefu huo baadhi yao kutoka katika familia
zenye uwezo mkubwa hulazimika kwenda kusoma mikoa mingine ambayo ipo mbali kwa
kutumia gharama kubwa, hivyo serikali imeombwa kunusuru hali hiyo kwa kujenga
shule ya watu wenye ulemavu wilayani humo.
Hayo yalisemwa na Katibu mkuu wa Chama Cha Walemavu (CHAWATA)
wilayani Mbinga Kassian Nyandindi, wakati alipokuwa akisoma risala ya watu
wenye ulemavu hivi karibuni mbele ya mgeni rasmi Mkuu wa wilaya hiyo Senyi
Ngaga, katika siku ya maadhimisho ya sherehe za watu hao zilizofanyika kijiji
cha Luhagara kata ya Litumbandyosi wilayani humo.
Wakati akisoma taarifa hiyo alisema bado kundi hilo
linakabiliwa na tatizo la miundo mbinu ya majengo mbalimbali kutokuwa rafiki
kwao na gharama kubwa ya viungo bandia kuwa bei ghali na kufikia hatua wengi
wao hushindwa kuvinunua.
Vilevile watu wenye ulemavu wilayani humo wamelalamikia
kukosa uwakilishi kuanzia ngazi ya mtaa, vitongoji mpaka kwenye vikao vya
Madiwani (Full Council) ili uwakilishi huo uweze kutetea haki zao za msingi.
Kwa upande wake akijibu risala hiyo Mkuu wa wilaya ya Mbinga
Senyi Ngaga, alisema matatizo hayo ameyapokea hivyo kwa yale ambayo yapo ndani
ya uwezo wa wilaya hiyo yatafanyiwa kazi, na mengine ambayo yapo nje ya uwezo
yatafikishwa ngazi ya juu serikalini kwa ajili ya utekelezaji zaidi.
Pia Ngaga aliwataka Wazazi na walezi wilayani humo, kuendelea
kuwathamini na kuwajali watu wenye ulemavu kwa kuwapatia mahitaji au huduma
muhimu ili baadaye waweze kujitegemea.
“Ndugu zangu walemavu ni Watanzania wenzetu hivyo
tunalojukumu la kuwa nao pamoja kwa kuwashirikisha katika shughuli za kimaendeleo
na sio kuwatenga au kuwaficha ndani, mzazi atakayebainika kufanya hivi serikali
itamchukulia hatua za kisheria”, alisema Ngaga.
Kadhalika aliongeza kuwa ni muhimu wapelekwe shule kwa kile
alichoeleza kuwa wengi wao, wanaouwezo mkubwa wa kufanya vizuri endapo wanapewa
nafasi au fursa mbalimbali.
No comments:
Post a Comment