Na Mwandishi wetu,
Songea.
WAKAZI wa mkoa wa Ruvuma
wameombwa kuunga mkono juhudi mbalimbali za wawekezaji wanaokwenda
kuwekeza katika mkoa huo, badala ya kubeza kwani hali hiyo inaweza kuwakatisha
tamaa wawekezaji hao na hatari ya kubaki watazamaji na
mabingwa wa kusifia maendeleo yaliyopo kwenye mikoa mingine.
Wito huo umetolewa mjini Songea na
mfanyabiashara Abbas Hemani wakati akizungumza na Mwandishi wetu, kuhusu
fursa nyingi za uwekezaji zilizopo katika mkoa wa Ruvuma na kuongeza kuwa iwapo
wakazi wa mkoa huo hawataunga mkono juhudi hizo basi mkoa huo,
utabaki na umasikini licha ya kuwepo kwa fursa na rasilimali nyingi.
Abbas ambaye ni wakala wa
shirika la ndege la AURIC AIR ambalo ndege zake hufanya safari kati ya Dar es slaam
na Songea mkoani humo, amewaomba wakazi wa mkoa huo hususani wafanyabiahara
kutumia usafiri wa ndege za kampu8ni hiyo, ili kumuunga mkono katika jitihada
zake za kutaka mkoa wa Ruvuma unakuwa miongoni mwa mikoa yenye
usafiri wa uhakika na kusaidia kuleta
maendeleo.
Alisema lengo la kuanzisha usafiri
huo wa ndege ni kuisaidia serikali katika kuboresha baadhi ya huduma
ambazo yenyewe ilishajitoa, hivyo kutoa nafasi kwa wananchi wenye uwezo
waweze kuwekeza katika maeneo mbalimbali kwa lengo la kuwahudumia
wananchi.
Mkoa wa Ruvuma ni miongoni mwa
maeneo ambayo usafiri wa kufika makao makuu ya nchi jijini Dar es slaam
kwa viongozi, wafanyabiashara na wananchi wengine ulikuwa mgumu kutokana na
umbali uliopo ambapo ni zaidi ya kilometa 1000 lakini tangu kuanza kwa safari
za ndege hizo, imekuwa rahisi kwao kufika maeneo mengine kwa ajili ya
shughuli mbalimbali ambazo siku za nyuma ilikuwa ni vigumu.
Aliongeza kuwa ndege hiyo yenye
uwezo wa kubeba abiria 25 hutumia muda wa masaa mawili kutoka Dar es
slaam hadi Songea, na sasa tayari katika miezi mitatu mfululizo imekwishasafirisha
zaidi ya watu 400 na matarajio yake kuwa itaongeza idadi, iwapo tu kutajitokeza
mahitaji makubwa kutoka kwa wananchi.
Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu amepongeza
jitihada za wakala huyo na kampuni ya AURIC AIR kwa kukubali kuanzisha
usafiri wa ndege mkoani Ruvuma, ukizingatia kwamba ni muda mrefu walikuwa na
mahitaji ya usafiri huo lakini hakuna kampuni yoyote iliyokubali kuleta
ndege zake licha ya jitihada za mara kwa mara kwa makampuni ya ndege kuyaomba
kufanya hivyo.
Naye mfanyabiashara maarufu wa
mjini Songea Mohamed Hussen, alieleza kuwa hivi sasa wanajivunia kuwepo kwa
usafiri huo katika kuboresha biashara zao, na hata ikitokea mteja anahitaji
bidhaa ambazo zipo mbali inakuwa rahisi kuagiza au kufuatilia tofauti na siku
za nyuma kabla ya kuanzishwa kwa usafiri huo wa anga.
No comments:
Post a Comment