Na Muhidin Amri,
Ruvuma.
SERIKALI mkoani Ruvuma imewaagiza Wakurugenzi
wa Halmashauri za wilaya katika mkoa huo, kutowapa tena zabuni Wakandarasi
ambao ni wababaishaji, wazembe na wenye rekodi mbaya katika utendaji wa kazi
zao, ili wasiweze kuisababishia serikali hasara ya kuingia gharama nyingine
upya ya ujenzi wa miradi ya Wananchi.
Mkuu wa mkoa huo Said Mwambungu
aliyasema hayo mwishoni mwa wiki wakati akifungua kikao cha siku moja cha Wajumbe
wa jumuiya ya serikali za mitaa(ALAT) kilichofanyika mjini Namtumbo mkoani
humo, ambapo alitumia nafasi hiyo kupiga marufuku wakandarasi wasiokuwa na sifa
kuomba na kufanya kazi katika mkoa wa Ruvuma kwani wamekuwa wakiurudisha nyuma
maendeleo ya taifa letu kwa ujumla.
Mwambungu amesikitishwa na usimamizi
mbovu wa fedha zinazotolewa na serikali wakati wa utekelezaji wa miradi mbalimbali,
ambapo imebainika kuwa wakandarasi wengi wamekuwa na tabia ya wizi kwa kuingia
mikataba hewa na halmashauri husika na wakishapata fedha hukimbia bila kukamilisha
kazi walizoomba kufanya, tatizo ambalo alidai kuwa linachangiwa kwa kiasi
fulani na baadhi ya watumishi hasa wakuu wa idara wasiokuwa waaminifu.
Alisema ni kosa kumpa kazi Mkandarasi
mwenye rekodi mbaya huku akiwaonya Wakurugenzi na Wenyeviti wa Halmashauri
juu ya tabia ya kuwa na urafiki wa jirani na wakandarasi hao kwa kile alichoeleza
kuwa kinatokana na tamaa ya fedha huku akisisitiza ni vema kutoa
kipaumbele kwa wakandarasi waaminifu na wenye sifa ambao wanatimiza
majukumu yao ya kazi kwa viwango vinavyotakiwa.
“Serikali haiwezi kuwavumilia
wakurugenzi, wenyeviti na hata wakandarasi wa aina hii ambao kila kukicha
kazi yenu ni kutafuta kuiba na kufanya mambo kwa maslahi yenu, tabia hii kwa
kweli hatuwezi kufika mbali kwani mnachangia sana kurudisha nyuma
maendeleo katika mkoa wetu”, alisema Mwambungu.
Alibainisha kuwa sio kosa kwa
Mkurugenzi wa Halmashauri na Mwenyekiti wakwe kuwa na urafiki na wakandarasi,
lakini uhusiano wao usiwe chanzo cha kushindwa kukemea au
kumchukulia hatua iwapo mtu aliyempa
kazi atashindwa kutimiza majukumu yake.
Aidha Mkuu huyo wa mkoa ametaka kasi
ya ukusanyaji mapato ya ndani katika Halmashauri kuongezeka kwani
hivi sasa hakuna hata halmashauri moja katika mkoa huo inayokusanya
kufikia asilimia 4 kati ya asilimia 100 hivyo kutegemea fedha kutoka
serikali kuu kwa ajili ya miradi na shughuli nyingine za maendeleo jambo
ambalo ni vigumu kuharakisha maendeleo ya wananchi.
Kadhalika Mwambungu amezitaka
Halmashauri mkoani Ruvuma, kuimarisha na kusimamia vizuri vyanzo vilivyopo vya
mapato ili viweze kuleta tija kama ilivyokusudiwa na serikali, kwa lengo la
kutaka kuboresha huduma mbalimbali za kijamii.
No comments:
Post a Comment