Na Steven Augustino,
Tunduru.
CHAMA kikuu cha ushirika Wakulima wa korosho wilaya ya Tunduru (TAMCU) mkoani Ruvuma, kimefanikiwa kukusanya tani 554 ambazo ni kidogo, kati ya tani 9115 zilizokadiriwa kuzalishwa katika msimu wa mwaka huu.
Hayo yalisemwa na Katibu mkuu wa chama hicho wilayani humo,
Imani Kalembo akiwemo na Mwenyekiti wake Mahamudu Katomondo mbele ya waandishi
wa habari, waliokuwa wakifanya mahojiano nao mjini hapa juu ya maendeleo ya
uzalishaji wa zao hilo.
Viongozi hao walifafanua kwamba wamepata wakati mgumu
kukusanya takwimu hizo za uzalishaji, kwa kile walichoeleza kuwa kutokana na wilaya
hiyo kuwa na utaratibu mbovu uliotumika kununulia zao hilo katika msimu wa
mwaka huu.
"Takwimu tulizowapeni ni zile ambazo tu zimetokana na
manunuzi yaliyofanywa na TAMCU kupitia vyama 18 vya ushirika vya wakulima ambavyo
vipo katika tarafa za Lukumbule, Namasakata, Nalasi, Matemanga, Mlingoti Nakapanya
na Namtumbo ambako chama kilipeleka fedha kwa ajili ya ununuzi wa Korosho",
alisema Kalembo.
Kadhalika viongozi hao walipongeza maamuzi ya serikali kwa
kuruhusu mfumo wa soko huria, kutumika katika msimu huu kutokana na wilaya ya
Tunduru wakulima wake kukosa wanunuzi katika misimu miwili iliyopita hali
ambayo ilisababisha kuwepo kwa malalamiko mengi kutoka kwa wakulima.
Walisema kupitia utaratibu huo msimu wa mwaka huu jumla ya makampuni
11 yalichuana kununua korosho wilayani humo, ambayo ni Export Trading company Limited,
Prayosa, Kulaathool company Limited, Shareeji Impex Limited, Said Mohamed Said
pamoja na Olam Tanzania Limited.
Makampuni mengine yaliyoomba kununua korosho kupitia mfumo wa soko huria ni China Pesticide
Tanzania Limited, Amina Seti, Saweya Impex Tanzania Limited, Alpha Choice Limited,
Sunrise Commodities pamoja na Chama kikuu cha ushirika cha wakulima wa korosho wilayani
Tunduru (TAMCU).
Pamoja na mambo mengine makampuni hayo yaliwekewa
utaratibu wa kuhakikisha kwamba yanafuata sheria na taratibu husika za manunuzi zilizowekwa, ikiwemo kununua zao hilo kutoka kwa wakulima kupitia vyama vya ushirika
pamoja na kulipa ushuru na kodi zote zilizoainishwa katika mikataba yao huku wakitakiwa
kutonunua kwa bei isiyopungua shilingi 1100.
No comments:
Post a Comment