Steven Augustino,
Tunduru.
SERIKALI wilayani Tunduru mkoani Ruvuma, imeweka mkakati wa
kuhakikisha kuwa kila kaya inakuwa na chakula cha kutosha wilayani humo ili
kuweza kuepukana na baa la njaa ambalo linaweza kutokea hapo baadaye.
Mikakati hiyo inaenda sambamba kwa kuanza kuwapeleka Mahakamani
watu wote, ambao hawatakuwa na mashamba ya kuzalisha mazao ya chakula katika
msimu wa mvua wa mwaka huu na kuendelea.
Chande Nalicho ambaye ni Mkuu wa wilaya hiyo, ndiye
aliyetangaza msimamo huo wa serikali na kuitaka jamii ya wanatunduru
kuhakikisha suala hilo linatekelezwa mara moja.
Kadhalika serikali itafanya mzunguko kwa kupita kutoa elimu
kwa wananchi wote wilayani Tunduru, na kwamba kesi za wavivu zichukuliwe hatua
kwa walengwa wanaoshinda vijiweni ikiwemo kufungwa.
Msimamo huo ulitangazwa na mkuu huyo wa wilaya, wakati alipokuwa
akizungumza katika mdahalo wa uzinduzi wa kampeni ya kutokomeza njaa duniani uliofanyika katika ukumbi wa Sky way, uliopo
mjini hapa.
Mdahalo huo ulihusisha viongozi wa madhehebu ya dini na kuungwa mkono juu ya
tamko hilo, ikiwemo kuundwa kwa sheria ndogo ambayo itafanya utekelezaji huo
uweze kuleta ufanisi.
Kwa ujumla wilaya ya Tunduru wakazi wake asilimia 84
wanategemea shughuli za kilimo, na katika mipango yake ya kawaida wilaya hiyo
imejiwekea mikakati ya kuzalisha mazao mengi ya chakula na biashara katika
msimu wa mwaka 2013 hadi 2014.
Akitoa ufafanuzi
katika mdahalo huo Askofu wa jimbo la Tunduru – Masasi, Castory Msemwa
alizitaka mamlaka na jamii kwa ujumla wanajenga ushirikiano katika kuhakikisha
lengo hilo linafikiwa ipasavyo na kuzaa matunda.
Alisema kutokana na ukosefu wa elimu, vitendea kazi, pembejeo
za uhakika na utawanyaji miundombinu yake ambao umekuwa usioaminika vimekuwa ni
kati ya vikwazo vikubwa katika jamii kukosa chachu ya maendeleo katika sekta ya
kilimo.
Askofu Msemwa pia aliwataka wananchi kuungana na shirika la
Caritas lililopo jimboni humo, katika kukabiliana
na upungufu wa chakula ambao unaweza ukajitokeza hapo baadaye.
No comments:
Post a Comment