Na Kassian
Nyandindi,
Mbinga.
VIONGOZI wa Chama cha kuweka na kukopa (SACCOS) wilayani
Mbinga mkoa wa Ruvuma, wametakiwa kujenga ukweli na uwazi katika utendaji wa
kazi zao za chama, na sio kutoa taarifa zisizo sahihi kwa wanachama ambazo
baadaye zinaweza kusababisha migogoro isiyokuwa ya lazima.
Aidha wametakiwa kutuoa ushirikiano wa kutosha kwa Mamlaka husika
ambayo inasimamia vyama vya ushirika, kufanya ukaguzi na kutoa hali halisi ya
mwenendo wa chama kwa wanachama, ili waweze kuwa na uhakika wa usalama wa mali
zao.
Rai hiyo ilitolewa na Ofisa elimu Msingi wilaya ya Mbinga,
Mathias Mkali alipokuwa mgeni rasmi kwenye mkutano mkuu wa chama cha kuweka na
kukopa cha Mbinga Kurugenzi SACCOS, uliofanyika kwenye ukumbi wa Jimbo la
Mbinga uliopo mjini hapa.
Vilevile aliwashauri wanachama wa umoja huo, wahakikishe kuwa
wanarejesha mikopo waliyokopa kwa wakati ili chama kiweze kusonga mbele.
“Napenda niwashauri, tujenge tabia ya kurejesha mikopo
tunayokopa kwa wakati uliopangwa na tukifanya hivyo chama hiki kitakuwa na
mzunguko mzuri kifedha, pia ili tuweze kufanikiwa jambo hili elimu ya ushirika itolewe
kwa wanachama”, alisema Mkali.
Awali kwa upande wake Meneja Mkuu wa Mbinga Kurugenzi Saccos,
Raymond Mhagama alisema chama hicho kwa kipindi cha mwaka huu kuanzia mwezi Januari
hadi sasa, kimeweza kutoa mikopo yenye thamani ya shilingi milioni 190,503,000.
Pia Mhagama alifafanua kuwa katika kipindi hicho wameweza kurudisha
akiba, amana na hisa zenye thamani ya shilingi milioni 110.3 kwa wanachama
waliokoma uanachama wao.
No comments:
Post a Comment