Na Kassian
Nyandindi,
Mbinga.
MKUU wa
wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Senyi Ngaga amemshukia Katibu wa Chama cha
Walimu Tanzania (CWT) tawi la Mbinga Samwel Mhaiki, akidai kwamba ni kikwazo
cha maendeleo ya elimu wilayani humo, kutokana na katibu huyo kupenda kuendesha
migogoro na kuchonganisha walimu mashuleni.
Ngaga
alisema hayo alipokuwa akizungumza na Wadau wa elimu, Kata ya Mbinga mjini juu
ya kukuza maendeleo ya sekta ya elimu wilayani humo, katika hafla fupi
iliyofanyika ukumbi wa Umati uliopo mjini hapa.
Alisema kuwa katibu huyo
amekuwa kinara namba moja wa kupita mashuleni na kushinikiza walimu waache
kufundisha (Wagome) hadi watakapolipwa madai yao, jambo ambalo alilieleza kuwa
limekuwa likileta mgogoro usio na tija katika jamii.
Alieleza
kwamba licha ya Mhaiki kuitwa mara nyingi ofisini kwake na kumtaka aache
kuendeleza migogoro hiyo, anashangaa kumuona bado akiifanya.
“Tumemuonya
mara nyingi huyo Mhaiki, lakini amekuwa bado akitusumbua kwa kuandika mabarua
na kusambaza mashuleni akishinikiza walimu wagome waache kufundisha….tulimwambia
serikali inashughulikia madai ya hawa walimu na watalipwa malumbano haya
anayoyaendeleza sasa ningelikuwa na uwezo mimi kama Mkuu wa wilaya hii
ningemhamisha, kwa sababu ni kikwazo kwa maendeleo ya elimu hapa wilayani, leo
walimu wakigoma watoto wetu watafundishwa na nani”, alisema Ngaga.
Mkuu huyo wa wilaya awali
alisema wilaya hiyo hivi sasa imejipanga katika kukuza kiwango cha elimu kwa
shule za msingi na sekondari, ambapo kwa kushirikiana na ofisa elimu wa wilaya
hiyo Mathias Mkali wamekuwa wakiendelea na mfumo wa watoto kujisomea wakati wa
likizo (Makambi) kwa kila kata wilayani humo, hususani kwa watoto wa darasa la
sita ambao wanaingia darasa la saba mwakani.
Alisema wazazi wameitikia
wito kwa kiasi kikubwa juu ya suala hilo na kukubaliana kutoa michango ya
chakula, katika vituo hivyo ambavyo watoto wao wanasoma wakati huu wa likizo.
Alisisitiza kuwa mtu yeyote
atakayeonekana anakwamisha mikakati waliyojiwekea ya kukuza kiwango cha elimu
wilayani Mbinga, yupo tayari kumwajibisha ili iwe fundisho kwa wengine wenye
tabia kama hiyo.
No comments:
Post a Comment