Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha
Walimu Tanzania (CWT) Ezekiah Oluoch amejikuta akiwa katika wakati mgumu, baada
ya kupokelewa na wanachama wa chama hicho wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, kwa
malalamiko ya hapa na pale na mabango yaliyobeba ujumbe wa aina mbalimbali
ambayo yalikuwa yakiwashutumu Katibu wa CWT wa mkoa huo na Wilaya hiyo.
Waliokuwa wakishutumiwa ni Zebedayo
Mwasandungila ambaye ni Katibu wa CWT mkoa wa Ruvuma na Samwel Mhaiki, Katibu
wa chama hicho wilayani Mbinga ambao wanalalamikiwa kutengeneza makundi ndani
ya chama.
Vilevile Mhaiki alikuwa akinyoshewa
kidole kwamba yeye na kamati yake ya chama wilayani humo, wameshindwa kukiongoza
chama na badala yake makato wanayokatawa wanachama ya asilimia 15 katika
mishahara yao hawarejeshewi katika matawi yao, hivyo hawaoni sababu ya
kuendelea kubaki na viongozi hao na kuwataka wajiuzuru mara moja.
Walisema wamekwisha mpatia Bw.
Mhaiki notisi ya siku 30 kwa lengo la kusudio la kumfikisha Mahakamani ili haki
zao ziweze kupatikana.
“Tumekwisha mwona mwanasheria kwa
lengo la kusudio la kumfikisha Mahakamani ndugu Samwel Mhaiki, na sasa
tumempatia notisi ya siku 30 atuambie fedha zetu za makato ya kila mwezi zipo
wapi”, walisikika wakisema kwa sauti.
Aidha Wanachama hao walikuwa
wakiendelea kupaza sauti wakisema Mwasandungila amekuwa akiwatumia meseji za
matusi pale wanapodai haki zao za msingi na kuwatishia usalama wa maisha yao.
Kwa upande wa Mhaiki walieleza kuwa
ameshindwa kuwaongoza na anatumia madaraka yake pasipo kuzingatia taratibu na
sheria zilizowekwa katika chama, hivyo hawana sababu ya kuendelea kuwa naye
hapa wilayani hivyo aondoke naye.
Wakati Naibu Katibu Mkuu Oluoch akisikiliza
kilio cha Wanachama hao kwenye ukumbi wa jumba la maendeleo uliopo mjini hapa,
huku wakimtaka asome ujumbe wa mabango waliyoyabeba ghafla alionekana kuwa
mkali na kukataa kuyasoma na kusema twendeni tuingie ukumbini tuzungumze siwezi
kuyasoma haya mabango yenu.
Kwa ujumla mabango yaliyokuwa
yamebebwa na wanachama hao yalikuwa yamebeba ujumbe uliokuwa ukisomeka kwamba;
karibuni Mbinga kwenye ufisadi, Mwenyekiti wa CWT ajiuzulu Mbinga sio msaada
kwetu, tunahitaji Katibu atakaye kiimarisha chama na sio mbabaishaji, tumechoka
na meseji za kashfa na matusi za Mwasandungila na Mhaiki hatukutaki wilaya ya
Mbinga wewe ni mzigo.
Baada ya Wajumbe kuingia ukumbini
hali ilikuwa sio shwari ambapo wanachama hao waliendelea kumweleza Naibu Katibu
Mkuu wa CWT Taifa Bw. Oluoch kwamba, wamekwisha wasilisha barua zao za kujitoa
uanachama na sasa wamefikia jumla yao 547 ambao wanatoka katika maeneo
mbalimbali wilayani Mbinga na huku wakiongeza kuwa wengine bado wanaendelea
kujiandikisha kwa ajili ya kujitoa.
“Mheshimiwa Naibu Katibu mkuu,
tumeandika barua za kujitoa uanachama na kusitisha makato mara moja katika
mishahara yetu yasiendelee kufanyika, tunachodai ni madai yetu ambayo tunakidai
chama toka mwaka 2011 tumechoka na hawa watu na sasa ondoka nao”, alisema
Edmund Hyera mwalimu wa shule ya msingi Juhudi kata ya Kigonsera.
Akisoma taarifa kwa niaba ya
Wanachama wenzake mbele ya Naibu Katibu Mkuu Taifa, Mwalimu Stella Mhagama
kutoka shule ya msingi Mtua kata ya Mpepai alisema wamechoshwa na vitendo
vinavyofanywa na kamati tendaji ya CWT wilayani Mbinga kwa kutengeneza migogoro
kati ya walimu na mwajiri wao, kwa kuandika mabarua ya kuchafuana na kuyapeleka
kwa viongozi wa ngazi ya juu.
Pia Mhagama alisema, wamechoshwa na
kamati hiyo kwa kile alichoeleza kuwa imekuwa ikitumia lugha za kashfa kwa
Wanachama pale wanapohitaji maelekezo muhimu ya kichama kutoka kwao kwa nyakati
tofauti.
Alieleza kuwa licha ya Wanachama
kuandika barua za malalamiko na kuzipeleka makao makuu ya CWT Taifa, hakuna
utekelezaji uliofanyika hivyo wao wamechoshwa na tabia inayofanywa na viongozi
wa chama hicho hapa wilayani na kusema, hawaoni sababu ya kuendelea kuwa
wanachama badala yake watajitoa.
Pamoja na mambo mengine akijibu hoja
za malalamiko ya Wanachama hao Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Walimu Taifa,
Ezekiah Oluoch alikiri ofisi yake kupokea malalamiko hayo akisema……….“ndugu
zangu wanachama kwanza kabisa mimi naomba niwaombee radhi hawa viongozi
waliowakosea kwa haya yote yaliyojitokeza hapa kwenu wilayani”.
Oluoch alisema ni kweli Katibu wa
mkoa na wa wilaya hiyo wanamakosa na ndio waliosababisha kuwepo kwa changamoto
hizo hivyo wamwachie yeye anakwenda kuyafanyia kazi kwa kukaa na viongozi
wenzake wa makao makuu ya chama.
“Dawa nzuri kwa haya yote
yaliyojitokeza kwa mtu muungwana ni kuomba radhi kwa matatizo haya niliyoyaona,
kwa niaba yao naomba niwaombee radhi na hawa walimu 547 msijitoe kwanza acheni
hiyo njooni tukijenge chama”, alisema Oluoch.
Alifafanua kuwa kinachotakiwa
viongozi wa CWT mkoani humo wametakiwa kuwa makini na utekelezaji wa majukumu
yao ya kazi na sio wakati wote kuchochea vurugu ambazo zinarudisha nyuma
maendeleo ya chama.
Hata hivyo alisema hivi sasa chama
hicho kimeweka utaratibu wa kuzunguka nchi nzima na kutoa semina kwa walimu,
ili waweze kutambua haki zao za msingi katika chama jambo ambalo litasaidia
kuondoa migogoro isiyo kuwa ya lazima.
No comments:
Post a Comment