Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
WANAWAKE wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma wametakiwa kuwa
makini katika kuendesha maisha yao kwa kujishughulisha na kilimo, biashara na
kujiunga na vyama vya akiba na mikopo ili waweze kuepukana na kujiingiza kwenye
anasa ambazo zinachangia maambukizi ya virusi vya ukimwi.
Sambamba na hilo wameshauriwa kushirikiana na kuchukua hatua
katika kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazowakabili katika maisha yao ya
kila siku kwa kufanya kazi kwa bidii.
Rai hiyo ilitolewa jana na Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake
Tanzania (UWT) wilayani Mbinga Pendo Ndumbaro, alipokuwa akizungumza na akina
mama waliolazwa katika hospitali ya wilaya hiyo iliyopo mjini hapa ambao
aliwatembelea kwa lengo la kuwataka hali na kuwapa zawadi mbalimbali.
Pia Mwenyekiti huyo alikuwa ameambatana na wanachama wenzake wa
umoja huo ambao walishiriki kwa pamoja kwenda kuwaona wagonjwa hao waliokuwa
wamelazwa katika hospitali hiyo.
“Ndugu zangu Mungu akitusaidia baada ya kupona ni wakati sasa wa
kujituma na kufanya kazi kwa bidii, wanawake wengi tumekuwa
tukijiingiza kwenye anasa kutokana na kutokuwa na ajira kama njia ya kujipatia
kipato, yatupasa tubadilike tuachane na mambo haya”, alisema.
Alisema huu ni wakati wa wanawake kujikwamua kiuchumi ikiwemo pia
kwa kujiunga kwenye SACCOS ambazo zitawasaidia kuwajengea uwezo kwa kupata
mikopo ya kuanzisha na kuimarisha miradi yao.
Kadhalika alieleza kuwa wanawake wanapaswa kujiendeleza kielimu na
kupambana na maisha kwa kufanya shughuli za kimaendeleo, badala ya
kushindana kwa mambo yasiyo na msingi.
Aliwataka wanawake kutambua kuwa wao ni kiungo muhimu
katika jamii hivyo ni vyema serikali, ikawawekea vipaumbele mbalimbali ili
waweze kujikwamua kimaisha kwa kuwa asilimia kubwa wao ndio walezi wa familia.
No comments:
Post a Comment