Wednesday, January 8, 2014

WATUHUMIWA MAUAJI YA MLINZI WA GAPCO WAPANDISHWA KIZIMBANI

Watuhumiwa wanaodaiwa kumuua mlinzi wa kampuni ya GAPCO inayouza mafuta wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, wakipandishwa katika Karandika la Polisi baada ya kusomewa mashtaka yao katika Mahakama ya wilaya hiyo leo. (Picha na Kassian Nyandindi)










Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

WATU watano wakazi wa Mbinga mjini mkoani Ruvuma, wameburutwa katika Mahakama ya wilaya ya Mbinga mkoani humo kwa tuhuma ya mauaji ya mlinzi wa kituo cha kuuza mafuta GAPCO, kilichopo mjini hapa.

Mwendesha mashtaka wa Polisi Inspekta Nassib Kassim alidai mbele ya Hakimu wa Mahakama ya wilaya hiyo, Joackimu Mwakyolo kuwa tukio hilo lilitokea Desemba 31 mwaka huu majira ya usiku.

Kassim aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Thito Turuka (30), Boniface Nombo (40), Ally Aman Chinga (29), Egno Nchimbi (24) na Felix Turuka (38).

Alidai Mahakamani hapo kuwa Watuhumiwa hao walimuua mtu aitwaye Kelvin Moyo (52) ambaye ni mlinzi wa kampuni hiyo, kwa kumkata koromeo na kumjeruhi vibaya sehemu mbalimbali za mwili wake.

Washtakiwa hao baada ya kusomewa shtaka linalowakabili, hawakutakiwa kujibu chochote kutokana na Mahakama hiyo kutokuwa na mamlaka ya kusikiliza kesi za mauaji.

Awali kabla ya Washtakiwa kusomewa shtaka hilo la mauaji, waliiomba Mahakama wasisomewe mpaka watakapo onana na Mkuu wa wilaya ya Mbinga, Senyi Ngaga wakidai kwamba Polisi wamewabambika kesi hiyo baada ya kukosa kukamata wahusika wa tukio hilo.

Walisema wamefanya hivyo kwa lengo la wao waonekane kwamba wamejivua lawama ionekane wamefanya kazi,  huku Mshtakiwa Thito Turuka (30) aliendelea kuiambia Mahakama kuwa Mkuu wa polisi wa wilaya hiyo aliyemtaja kwa jina la Justine Joseph, aliwatamkia wakati wakiwa mahabusu ya polisi kwamba lazima wakasote miezi sita gerezani.

“Mheshimiwa Hakimu, sisi tunashangaa tulikamatwa watu wengi lakini wenzetu baadhi yao wametoa fedha na kumpatia huyu OCD na kuachiwa huru, ushahidi tunao tunaomba tupate muda tupeleke malalamiko haya kwa mkuu wa wilaya”, alisema Turuka.

Pamoja na mambo mengine, Hakimu Joackimu Mwakyolo aliwajibu Washtakiwa hao kwamba wafuate taratibu kwa kuandika barua kwenda kwa Mkuu wa gereza la Mahabusu Mbinga mjini, wakimuomba kuonana na Mkuu huyo wa wilaya ili waweze kumweleza malalamiko yao.

Hata hivyo shauri hilo litakuja kusikilizwa tena Januri 21 mwaka huu, na kwamba washtakiwa wamerudishwa mahabusu.

No comments: