Gaudence Kayombo. |
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
MBUNGE wa jimbo la Mbinga Gaudence
Kayombo amesema, ujenzi wa barabara
kiwango cha lami kuanzia eneo la Likuyufusi pacha ya Peramiho wilaya ya Songea
hadi Mbinga, katika baadhi ya maeneo umejengwa kwa kiwango kisichoridhisha
kutokana na barabara hiyo kuanza kuwekwa viraka kabla ya kukabidhiwa rasmi
mikononi mwa serikali.
Kayombo alisema hayo alipokuwa
akizungumza na mwandishi wa habari hizi mjini hapa, huku akisisitiza kuwa hali
hiyo huenda ikatokana na wataalamu husika kutozingatia ipasavyo vipimo vya
kimaabara na ndio maana barabara hiyo hubomoka na kulazimika kuweka viraka.
Alisema uzembe huo uliofanywa wa
kutozingatia viwango husika ni hasara kubwa kwa serikali kutokana na fedha
nyingi iliyotumika kujengea barabara hiyo kutofanya kazi yake kama
ilivyokusudiwa.
“Barabara ya kutoka Songea kwenda
Namtumbo imejengwa vizuri sana haina viraka, ni jambo la kusikitisha sana
barabara hii ya kwetu toka Songea kwenda Mbinga bado haijakamilika ujenzi wake
leo tunaanza kuweka viraka, kweli tutaweza kudumu nayo kwa miaka mingi ?
”, alihoji Kayombo.
Kwa ujumla barabara hiyo ambayo ni
ya kilometa 78 inagharimu kiasi cha shilingi bilioni 79.8 na sasa ipo katika
hatua za mwisho kukamilika ujenzi wake.
Fedha za ujenzi huo ni miongoni mwa
dola 698 za Kimarekani zilizotolewa nyakati za mwisho katika utawala wa Rais
mstaafu George Bush, ikiwa ni sehemu ya msaada kwa ajili ya kujenga miradi
mbalimbali ya kimaendeleo hapa nchini.
Kampuni ya Sinohydro Corporation
Limited kutoka nchi ya China, ndiyo imekabidhiwa kazi ya ujenzi wa kiwango cha
lami na kwamba ujenzi wake ni wa miezi 27.
Hata hivyo ni mradi mkubwa wa pili
hapa mkoani Ruvuma, wa ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami ambao
umetanguliwa na mradi mwingine wa ujenzi wa barabara ya lami kutoka Songea hadi
Namtumbo ikiwa ni utekelezaji wa maendeleo ukanda wa Mtwara.
No comments:
Post a Comment