Saturday, May 31, 2014

WATAKIWA KUONGEZA JUHUDI KATIKA MASOMO



Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

WANAFUNZI wa shule  ya sekondari  Agustivo iliyopo katika wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma,  wametakiwa kuongeza juhudi katika masomo yao ili waweze kutimiza malengo waliyonayo katika maisha na kuacha kujiingiza kwenye mambo yatakayowaharibia malengo yao.


Ushauri huo umetolewa na mfanyabiashara maarufu  mkoani Ruvuma Abbas Herman, alipokuwa akizungumza  na wazazi na wanafunzi kwenye mahafali ya kidato cha sita shuleni hapo huku akisisitiza umuhimu wa elimu.


Katika sherehe hizo za kuwaaga wahitimu wa kidato cha sita, mfanyabiashara huyo pia aliwazawadia wanafunzi 14  kiasi cha shilingi 25,000  kila mmoja  waliokuwa wamefanya vizuri katika masomo yao na  kiasi cha shilingi 1,000,000 kwa ajili ya shule hiyo ikiwa ni zawadi ya kufanya vizuri kitaaluma mkoani Ruvuma.

Monday, May 26, 2014

VIONGOZI CCM WANAOFANYA KAMPENI KABLA YA WAKATI KUCHUKULIWA HATUA ZA KISHERIA

Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Songea mkoani Ruvuma, Josephat Ndulango, akisisitiza jambo wakati alipokuwa akizungumza na Waandishi wa habari ofisini kwake. (Picha na Gwiji la matukio Ruvuma)

Na Kassian Nyandindi,
Songea.

CHAMA cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Songea mkoani Ruvuma, kimewataka viongozi wake kuacha kufanya kampeni kabla ya wakati na atakayebainika hatua kali za kisheria, zitachukuliwa ili iwe fundisho kwa wengine wenye tabia kama hiyo.

Sambamba na hilo kimewataka kuepukana na makundi, na badala yake kupitia mikutano ya wananchi waeleze utekelezaji wa ilani ya CCM ili kuweza kujenga misingi ya kukiimarisha chama, na wananchi waweze kutambua nini kimewafanyia.

Rai hiyo ilitolewa na Katibu wa Chama cha Mapinduzi wilaya ya Songea, Josephat Ndulango alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake juu ya mikakati ya kukiimarisha chama hicho.

Ndulango alisema Watendaji katika maeneo mbalimbali wilayani humo baadhi yao wamekuwa kikwazo katika kusukuma mbele maendeleo ya wananchi, hivyo wamesisitizwa kuacha kujiingiza kwenye mambo ya kisiasa badala yake wazingatie majukumu yao ya kazi.

Saturday, May 24, 2014

MAMLAKA YA CHAKULA NA DAWA YAZITAKA HALMASHAURI ZA WILAYA KUTEKELEZA MAJUKUMU YAKE IPASAVYO

Baadhi ya Wahariri na Waandishi wa habari wakiwa kwenye mkutano na TFDA katika ukumbi wa hospitali ya mkoa wa Mbeya.

 Mkurugenzi wa huduma za maabara kutoka Mamlaka ya chakula na dawa (TFDA) Charys Ugullum,(aliyesimama) akizungumza na Wahariri na Waandishi wa habari Jijini Mbeya wakati wa ufunguzi wa mkutano huo.

Baadhi ya Waandishi wa habari na Wahariri wa Nyanda za juu Kusini, wakiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Mamlaka ya chakula na dawa (TFDA). (Picha zote na Kassian Nyandindi)


Na Kassian Nyandindi,
Mbeya.

HALMASHAURI za wilaya hapa nchini kupitia kamati zake za udhibiti wa ubora wa chakula na dawa, zimetakiwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo ili kuweza kulinda afya za wananchi.

Rai hiyo ilitolewa na Mkurugenzi wa huduma za maabara kutoka Mamlaka ya chakula na dawa Tanzania (TFDA) Charys Ugullum alipokuwa akizungumza kwenye mkutano wa siku moja, Wahariri na Waandishi wa habari wa mikoa ya Nyanda za juu Kusini Jijini Mbeya.

Mkutano huo ulifanyika katika ukumbi wa Hospitali ya mkoa huo, ambapo ulilenga kuwaelimisha Wahariri na Waandishi wa habari  namna ya kuibua matatizo ya bidhaa feki ambazo huuzwa maeneo mbalimbali hapa nchini, kwa lengo la kuleta ufanisi na ubora wa chakula na dawa.

Sunday, May 18, 2014

ASKOFU MKUU WA JIMBO KUU LA SONGEA ASIMIKWA, AWATAKA WATANZANIA KUDUMISHA MUUNGANO

Askofu Mkuu wa Jimbo kuu la Songea mkoani Ruvuma, Damian Dallu.



















Na Kassian Nyandindi,

Songea.

ASKOFU mkuu wa Jimbo kuu la Songea mkoani Ruvuma, Mhashamu Damian Dallu amewataka Watanzania kuuenzi na kudumisha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambao umedumu kwa miaka 50 sasa, kwa manufaa ya wananchi wa pande zote mbili.

Pia alisema Watanzania waliungana kwa moyo wao wenyewe na sio kwa karatasi, hivyo wanaohangaika kutafuta karatasi zenye maelezo ya muungano huo, wanapoteza muda na kwamba mchakato wa katiba mpya usipewe nafasi ya kuuangamiza taifa hili.

Kauli hiyo aliitoa leo mara baada ya kumalizika kwa ibada ya kusimikwa kuwa Askofu mkuu wa jimbo hilo, ambalo lilikuwa wazi baada ya kujiuzulu aliyekuwa Askofu wake Norbert Mtega mwaka mmoja uliopita.

Sunday, May 11, 2014

NGAGA AWAWEKA KITIMOTO VIGOGO WA HALMASHAURI YA MBINGA

Na Muhidin Amri,

Mbinga.


MKUU wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Senyi Ngaga amegeuka mbogo na kuwaweka kiti moto baadhi ya vigogo wa wilaya hiyo kufuatia kuwepo kwa matokeo mabaya, yaliyopatikana kwenye maeneo wanayo yaongoza katika mtihani wa kumaliza elimu ya msingi mwaka jana. 

Ngaga alisema hali hiyo imesababisha wilaya hiyo kushika nafasi ya pili kimkoa  kinyume na maadhimio waliyojiwekea ya kushika nafasi ya kwanza  katika mtihani huo.

Hali hiyo ilijitokeza wakati wa kikao cha tathimini ya elimu ambapo Mkuu huyo wa wilaya hakuridhishwa na hali ya ufaulu katika kata zinazoongozwa na vigogo hao ambao ni Mwenyekiti wa chama cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Mbinga Christantus Mbunda, ambaye ni diwani wa kata ya Mbangamao.

Vilevile Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya hiyo Allanus Ngahy diwani wa kata ya Kipapa na diwani wa kata  ya Ngima Winfrid Kapinga ambaye ni makamu Mwenyekiti wa halmashauri hiyo ambaye pia ni diwani wa kata ya Ngima wote kupitia tiketi ya chama hicho.

Thursday, May 8, 2014

ASKOFU ALIA NA WANASIASA AWASIHI WATIMIZE MAJUKUMU YA WANANCHI KWANZA


Na Kassian Nyandindi,

Mbinga.

ASKOFU wa Jimbo Katoliki la Mbinga mkoani Ruvuma John Ndimbo, amewataka Madiwani wa wilaya ya Mbinga mkoani humo kuacha itikadi za kisiasa pale wanapotekeleza mambo ya msingi ya wananchi, na endapo wasipozingatia hilo huenda wakasababisha machafuko katika jamii.

“Mwanasiasa yeyote ambaye hana kanuni na hazingatii mambo ya msingi huyo anaipoteza jamii, tuache itikadi za kisiasa tutekeleze kwanza majukumu tuliyopewa na wananchi”, alisema Ndimbo.

Kauli hiyo ilitolewa na Askofu huyo katika kikao cha tathimini ya elimu kilichoketi hivi karibuni, kwenye ukumbi wa jimbo katoliki la Mbinga ambacho kilikuwa kikiendeshwa na Mwenyekiti wake Mkuu wa wilaya hiyo Senyi Ngaga.

Sunday, May 4, 2014

TATIZO LA MAJI MBINGA MBIUWASA YANYOSHEWA KIDOLE

Mkuu wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Senyi Ngaga.



















Na Kassian Nyandindi,

Mbinga.

UHABA wa maji ni tatizo ambalo limekuwa likiendelea kutesa Wakazi wa mji wa Mbinga mkoani Ruvuma, na kusababisha wakazi hao kuinyoshea kidole Mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira (MBIUWASA) iliyopo katika mji huo, ambayo ndio tegemeo kubwa katika utoaji wa huduma hiyo muhimu.

Kufuatia hali hiyo wameitaka Mamlaka kuhakikisha kwamba inatatua kero hiyo mapema, ili wakazi hao waweze kuondokana na adha wanayoipata sasa ya mgao mkali wa maji.

Walisema ni jambo la kushangaza mji huo kukosa maji kwa kile walichoeleza kuwa, ni kipindi cha masika na maji yamekuwa mengi kiasi ambacho hawakutakiwa kukumbwa na karaha hiyo, huku wakifafanua kuwa muda mwingi maji hayo ya mgawo yamekuwa yakielekezwa katika nyumba za vigogo huku watu wa kawaida wakiendelea kuteseka.

Malalamiko hayo yalitolewa kwa nyakati tofauti walipokuwa wakizungumza na Mwandishi wa habari hizi mjini hapa, huku wakidai kuwa wakati mwingine inawalazimu kufuata maji umbali mrefu katika vijito vidogo vidogo, ambavyo huzunguka mji wa Mbinga.

Friday, May 2, 2014

TATIZO LA MIMBA LATISHIA USTAWI WA MAENDELEO KATIKA SEKTA YA ELIMU MBINGA



Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

TATIZO la mimba mashuleni kwa shule za msingi na sekondari wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, lisipotafutiwa mbinu ya kudhibitiwa mapema, hakika maendeleo katika sekta ya elimu wilayani humo huenda yakadorola.

Imefafanuliwa kuwa wazazi na walimu katika shule husika ndio chanzo kikuu cha tatizo hilo ambapo kwa kiasi kikubwa, wamekuwa wakifumbia macho kwa kutowachukulia hatua za kisheria watu wanaohusika kuwapatia wanafunzi wa kike ujauzito.  

Wadau wa elimu wilayani Mbinga mkoani humo, walisema hayo mbele ya Mkuu wa wilaya hiyo Senyi Ngaga ambaye alikuwa Mwenyekiti katika kikao cha tathimini ya elimu, kilichoketi katika ukumbi wa Jimboni uliopo mjini hapa.