Mkuu wa wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma Ernest Kahindi, akiwa ofisini kwake wilayani humo. (Picha na Kassian Nyandindi) |
Na Kassian Nyandindi,
Nyasa.
SAKATA la mgogoro wa
kugombea ardhi na mipaka katika kitongoji cha Mshangano kijiji cha Liparamba
tarafa ya Mpepo wilayani Nyasa mkoa wa Ruvuma, limechukua sura mpya kufuatia
Wakazi wa maeneo hayo kumlalamikia Mkuu wa wilaya hiyo Ernest Kahindi huku
wakimnyoshea kidole kwamba ameshindwa kumaliza mgogoro huo kwa kufuata taratibu
husika ikiwemo ridhaa ya wananchi, badala yake anatumia nguvu kubwa
kunyanyasa viongozi wa kijiji hicho.
Wakizungumza na
mwandishi wa habari hizi kwa nyakati tofauti kijijini hapo, wakazi hao
walisema Kahindi amefikia hata hatua ya kumweka mahabusu kwa siku tatu katika
kituo kikuu cha polisi wilaya ya Nyasa, Mwenyekiti wa kijiji Joseph Komba bila
kosa lolote huku akizuia dhamana.
Uchunguzi umebaini
kuwa Mwenyekiti huyo aliwekwa mahabusu kuanzia siku ya Ijumaa Juni 20 na
kudhaminiwa Juni 23 mwaka huu majira ya jioni, ambapo kufikia saa 11 jioni siku
hiyo ndipo alichukuliwa maelezo na kuambiwa atafute mtu wa kumdhamini huku
akipewa usumbufu wa kuendelea kuripoti kila siku katika kituo hicho cha polisi.