Gaudence Kayombo Mbunge Mbinga Mashariki. |
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
WANANCHI siku zote wamekuwa wakiamini kwamba, kiongozi
yeyote aliyewekwa madarakani, ni mtetezi na msimamizi mkuu wa maendeleo yao katika eneo husika.
Kana kwamba hilo
halitoshi, baadhi yao wakishawekwa madarakani
wanaonekana kuwa mwiba kwa wananchi, na hata kutotimiza ipasavyo majukumu yao ya kazi.
Jamii siku zote hufikia hatua ya kupoteza imani kwa viongozi
wao endapo tu, pale wanapobaini msimamizi wao wa maendeleo tayari yupo katika
mrengo wa kushoto dhidi yao,
wakimuona akijijengea maslahi yake binafsi na kusahau wananchi anaowatumikia.
Tatizo hili likigundulika ndio maana utakuta migogoro
au malalamiko ya hapa na pale huanza kujitokeza, na kiongozi husika kunyoshewa
kidole wakati mwingine kusababisha kutokea kwa vurugu zinazoweza kuhatarisha
amani katika eneo husika.
Mwandishi wetu wa makala haya, anapenda kuelezea juu
ya mgogoro uliojitokeza katika kata ya Ruanda wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, ambapo Mbunge wa Mbinga Mashariki Gaudence
Kayombo hivi karibuni ametishia kujiuzuru wadhifa huo, kwa kile kinachodaiwa
kufuatia kushushiwa tuhuma nzito dhidi yake.
Tuhuma hizo zinatokana na wakazi wa kata hiyo
kumtuhumu Mbunge huyo kwamba anashindwa kuyafanyia kazi matatizo ya wananchi wa
kata hiyo kwa kile kinachodaiwa kwamba, kutokana na kuwa na mahusiano ya karibu
na mwekezaji wa mgodi wa makaa ya mawe Ngaka uliopo katika kijiji cha Ruanda katika
kata hiyo.
Tuhuma hizo za wananchi
ziliwasilishwa katika kikao cha
Halmashauri kuu ya Chama Cha Mapinduzi(CCM) kilichoketi Februari 26
mwaka huu, kwenye ukumbi wa jengo la Mfuko wa maendeleo ya jamii(TASAF) liliopo
katika kata hiyo.
Wajumbe wa kikao hicho ndio waliowasilisha tuhuma husika,
ambapo kikao kilikuwa kikiongozwa na Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Mbinga,
Christantus Mbunda na kwamba licha ya Mbunge Kayombo kupewa mwaliko wa
kuhudhuria kikao, lakini hakuweza kujitokeza na haikujulikana ni kwa sababu
gani.
Kwa mujibu wa vyanzo vya uhakika vimeendelea kueleza
kuwa pamoja na Mbunge huyo kuwa karibu na mwekezaji huyo, pia inadaiwa
amejengwa nyumba ya gorofa moja kijijini kwao Ruanda na kujimilikisha ekari 400
za ardhi katika kata ya Ruanda bila kufuata
taratibu husika.
Kayombo ni mzaliwa wa kijiji cha Ruanda kata ya
Ruanda, ambako ndiko hivi sasa uchimbaji na usafirishaji wa makaa ya mawe katika mgodi wa Ngaka umekuwa
ukiendelea kufanyika na mgodi huo, unamilikiwa na kampuni ya ubia ya Tancoal
Energy ambayo asilimia 30 ya hisa zake zinamilikiwa na serikali, kupitia
shirika la maendeleo la Taifa NDC na asilimia 70 ya hisa zinamilikiwa na
mwekezaji wa kampuni ya Intra Energy.
Baada ya kikao hicho kuwasilisha tuhuma hizo, imeelezwa kuwa Mbunge Kayombo alipigiwa simu na mmoja kati ya wajumbe
waliokuwepo katika kikao hicho(jina tunalo) wakimtaka waonane naye.
Kufuatia hilo Mbunge
huyo aliwajibu yupo safarini akitokea mjini Songea na kuelekea huko kijijini
kwao alikozaliwa, hivyo anaomba wamsubiri ili waweze kuzungumzia tatizo hilo.
Baadhi ya wajumbe walipoona muda mrefu unazidi kwenda
na hajitokezi, waliamua kuchukua uamuzi wa kuanza kurudi wakiwa katika gari lao
na kwamba kwa bahati nzuri wakiwa njiani walifanikiwa kuonana naye akitokea
safari yake aliyowaeleza ndipo wakaamua kusimama na kumueleza yaliyojiri katika
kikao hicho.
Chanzo chetu cha habari kinasema, Kayombo alipoelezwa
shutuma hizo alionekana kuwajia juu, huku akionesha kusikitishwa na kuwaeleza
wajumbe hayo ni malalamiko ambayo si ya kweli.
“Mheshimiwa Mbunge baada ya kusimama pale na kumweleza
hili alikuja juu na kusema, yeye nyumba wanayomtuhumu amejengewa na mwekezaji
alisema ameijenga mwenyewe na suala la kumiliki ardhi ekari 400 sio la kweli,
na alikana kwamba hana mahusiano yoyote ya karibu na mwekezaji wa mgodi huo”,
kilisema chanzo chetu ambacho kiliomba kisitajwe gazetini.
Habari zinaarifu kuwa eneo hilo ambalo walisimama kati
ya Kayombo na wajumbe waliotoka katika kikao hicho, hapakuwa na amani wala maelewano
hadi wana achana, kutokana na Mbunge huyo kung’aka na kujawa jazba huku
mwishoni akiwaeleza na kutishia wenzake kwamba ni vyema ajiuzuru kutokana na
kashfa wanazomtuhumu kutokuwa na ukweli.
Uchunguzi uliofanywa umebaini kuwa hadi
habari hizi zinaenda mitamboni, tayari jopo la uongozi wa CCM wilayani Mbinga
mnamo tarehe 1 mwezi Marchi mwaka huu, lilikwenda nyumbani kwa Kayombo kijijini
kwao na kumsihi asijiuzuru na inadaiwa kwamba huenda asijiuzuru pamoja ya kwamba
Mbunge huyo awali kuweka msimamo wa kutaka kuachia madaraka hayo.
Tumeendelea kubaini pia hilo,
linatokana na wakazi wa kata ya Ruanda wamekuwa wakilalamika kwa muda mrefu na
kupinga kusafirishwa kwa makaa hayo ya mawe ambayo yanachimbwa katika kijiji
cha Ntunduaro katika kata hiyo, wakitaka watekelezewe kwanza madai yao ya msingi ambayo
mwekezaji husika anaonekana kutoyatimiza.
Kwamba madai yao
ni nyongeza ya fidia zao katika eneo ambalo walihamishwa, kwa ajili ya kupisha
kazi ya uchimbaji wa makaa hayo na kupinga juu ya uchafuzi wa mazingira
yakiwemo maji katika mto Nyamabeva ambao unafanywa na wachimbaji wa madini
hayo.
Maji ya mto huo yamekuwa yakitumika na wananchi hao
kwa shughuli mbalimbali majumbani mwao, lakini hivi sasa wanashindwa kuyatumia
kutokana na wachimbaji wa makaa ya mawe
kutiririsha maji yenye mkaa kuelekea kwenye mto huo, na kusababisha baadhi ya
viumbe kama vile samaki kupoteza maisha.
Wakati hilo linatokea
serikali wilayani Mbinga licha ya kutuma wataalamu wake wa mazingira kwenda
huko na kufanya upembuzi yakinifu juu ya tatizo hilo, bado majibu ya uhakika juu ya madhara
ya maji hayo yaliyochanganyika na mkaa wa mawe, hayajatolewa kwa wananchi
wanaoishi jirani na mgodi huo.
Kamati ya ulinzi na usalama, hivi karibuni ilienda
kule na kuwatuliza tu wananchi wale na kutoa kauli kwamba madai yao yapo kwenye ngazi
husika yanashughulikiwa, baada ya kuonekana hali ya kutaka kuhatarisha amani
kati ya kampuni inayochimba mkaa huo, Tancoal Energy.
Pia jukumu lililochukuliwa na kamati hiyo ni kwenda
huko na kuamuru wachimbaji hao, kuzuia maji hayo yenye mchanganyiko na mkaa huo
yasielekezwe tena katika mto huo ili kunusuru maisha ya wakazi hao.
Mbunge wa Mbinga Mashariki Gaudence Kayombo alipoulizwa juu ya
tuhuma na malalamiko hayo, alisema yeye hawezi kuzungumzia lolote kwa sasa.
Vilevile ofisa ardhi na maliasili wa wilaya hiyo
Richard Mwaiseje, alipotakiwa kutolea maelezo juu ya Mbunge huyo kujimilikisha
ekari zaidi ya 5,000 za ardhi, alisema hana uthibitisho juu ya tuhuma hizo.
“Si dhani kama ni taarifa ya kweli, kwa sababu na sisi
tunalisikia tu hivyo mpaka nifanye utafiti kama
ni kweli anamiliki maeneo makubwa au vipi”, alisema Mwaiseje.
Kadhalika kumekuwa na vumbi kali la mkaa wa mawe
limekuwa likienea katika vijiji vilivyokuwa jirani na mgodi huo pale
unaposafirishwa kwenda bandari ya Ndumbi iliyopo katika ziwa Nyasa, Kiwira
mkoani Mbeya na kiwanda cha kuzalisha saruji Tanga kilichopo mkoani Tanga,
huenda hali ya kiafya kwa wananchi wale ikawa hatarini endapo hatua husika hazitachukuliwa
kwa uharaka.
Nimezungumza na baadhi ya wananchi wa kijiji cha
Ntunduaro ambao hawakutaka majina yao
yatajwe gazetini, wakidai kwamba wamechoshwa na ahadi ambazo hazizai matunda na
utekelezaji wake unaonesha ukifanywa taratibu licha ya hata Mbunge wao Gaudence
Kayombo kufikishiwa mezani kwake na hakuna hatua alizozichukua ndio maana leo
hii wanakosa imani naye.
Viongozi wa serikali wa kata ya Ruanda wamezungumza na
mwandishi wa makala haya kwa nyakati tofauti, wamesema ni kweli malalamiko hayo
yapo na hata kwa mbunge wao yamefikishwa na majibu yanayotolewa ni ahadi tu, kwamba
yanafanyiwa kazi huku siku zikiendelea kuyoyoma utekelezaji wake hauonekani.
Pia walisema kampuni ya Tancoal Energy ambayo inachimba mkaa huo kutokamilisha
kwa muda mrefu kazi waliyoahidi kuifanya ya ukarabati wa zahanati ya kijiji
hicho, ujenzi wa visima vya maji na shule, ni jambo ambalo limekuwa likizua
malalamiko yasiyo na msingi badala yake wamemtaka mwekezaji huyo atimize mambo
ya msingi ili kumaliza mgogoro huu uliopo sasa usiweze kuendelea.
Mwandishi wa makala haya ameshuhudia hata katika eneo
linalotumika na baadhi ya wafanyakazi wenye asili ya kitanzania, wamekuwa
wakitengwa ambapo wengi wao wamekuwa wakilalamika hawajajengewa vyoo na muda wa
chakula unapowadia hujisetiri katika eneo la wazi kutokana na kubaguliwa na
mwekezaji husika na kulazimika kutumia vyoo vya majirani wanaoishi kuzunguka
eneo lilipo ofisi za mgodi huo.
Madereva wanaoendesha magari ya kampuni hiyo ndio
wamekuwa wakitengwa kwa kiasi kikubwa,
ambapo walitolea mfano kwa gari aina ya Pickup mtanzania huruhusiwa
kupanda nyuma ya bodi la gari hilo ambalo liko
wazi, na katika sehemu nzuri ya gari katikati hubebwa mnyama aina ya nyani,
kitendo ambacho baadhi yao
wanasema ni ubaguzi uliokithiri.
Hata hivyo jitihada ya kumpata Meneja wa Tancoal
Energy Injinia Isaac Mamboleo, ili aweze kutolea ufafanuzi juu ya hali hii
inayolalamikiwa zilishindikana.
Binafsi nashauri kukalia kimya malalamiko ya wananchi ni
kutowatendea haki, kila mtu anapenda na kutaka kusifiwa lakini hakuna anayetaka
kupokea lawama au hata wajibu wa kuwajibika wengine wakifanya mabaya kwa niaba yao.
No comments:
Post a Comment